Pekua/search

Thursday, July 25, 2013

Serikali Tatu Zitapunguza Gharama za Uendeshaji



Serikali Tatu Zitapunguza Gharama za Uendeshaji

 Gharama za ziada zinaweza kuepukwa mathalan kwa kuiondosha Ofisi ya Makamu wa Rais na kuivunjilia mbali ofisi ya Waziri Mkuu butu asiye na meno hata kucha

Kinachoelekea kuuteka mjadala wa katiba mpya hivi sasa ni pendekezo la serikali tatu. Naunga mkono serikali tatu kwa kuwa kiuhalisia imethibitika kuwa vigumu kuwa na serikali moja kwa kisingizio cha kumezana. Na hizi mbili zimechusha kero zake na viraka vimekuwa vingi mno kiasi kwamba nguo yetu hii Muungano itatatuka pasipo kujitafakari upya.

Sababu kubwa inayoonekana kuwa nzito ni kuhusu gharama. Ninachangia hili la gharama kwenye makala hii fupi.

 Serikali tatu zinaweza kuokoa sana gharama ikiwa tutaacha hofu ya kisichojulikana na kujikita katika kufikiri kwa kutumia mbongo na sio visigino nk kama walivyofanya kina Nyerere na Karume walivyofikiri kwa mbongo zao na nia na dhati ya mioyo kabisa. Nasi sasa tunao wajibu; Tukiutimiza wajibu huu tutatuzwa na tukiutelekeza tutatwezwa maana ilishanenwa Likulli ajalin kitab', yaani kila zama ina kitabu chake,”

Gharama za ziada zinaweza kuepukwa mathalan kwa kuiondosha Ofisi ya Makamu wa Rais na kuivunjilia mbali ofisi ya Waziri Mkuu butu asiye na meno hata kucha (ofisi na sio mhe Pinda). Viongozi wakuu wa serikali hizi mbili yaani  Tanzania Bara na Zanzibar  ndiyo watakuwa wasaidizi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na mawaziri wachache wa kisekta watakuwa wasaidizi wa karibu wa viongozi wakuu wa serikali hizi mbili za Tanzania bara na Zanzibar .

Bajeti inayotumika sasa kuendesha ofisi ya Rais itatumika kuendesha ofisi ya Rais wa Muungano sambamba na kusimamia masuala ya Muungano. Gharama za uendeshaji wa ofisi ya Waziri Mkuu na sehemu ya bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Rais sasa zitatumika kuendesha Ofisi ya Kiongozi wa Serikali ya Tanzania Bara (bila kujali cheo cha kiongozi huyo ataitwaje). Bajeti za wizara ambazo si za muungano (hizo zipo hata sasa) hata hivyo zinaweza kupunguzwa.

Gharama za uendeshaji wa serikali ya Zanzibar wala haina haja hata kuhofia maana hizo zipo hata sasa.

Ni gharama zipi tunazozihofia kuongezeka katika kuendesha serikali tatu?

Kwa upande wa Bunge
Bunge la Muungano halitakuwa na haja ya kukaa muda mrefu kama ilivyo sasa kwani masuala ya muungano si mengi kiasi hicho. Gharama za muda utakaookolewa zitatumika kuendesha bunge la Bara. Hali kadhalika Bunge la Tanzania Bara litapungua ukubwa wake na hivyo kupunguza gharama tofauti na hivi sasa ambapo wakati wa kujadili masuala ya bara yasiyo ya muungano wabunge kutoka zanzibar huwa hawatoki wanakuwepo na posho wanalamba kama kawaida ilhali mijadala inayoendelea inahusu mambo ‘yasiyowahusu’.

Gharama gani tunazihofia? Mambo yasiyo ya Muungano kwa upande wa Visiwani yanajadiliwa na baraza la wawakili hata sasa. Serikali tatu zinaweza kupunguza gharama hata zile za vikao vya mapatano na kutanzua kero za muungano wa serikali mbili za sasa ambazo hazitanzukiki.

Friday, June 14, 2013

NAFASI ZA MASOMO YA KOZI ZA UALIMU- Chuo Kikuu cha Tumaini Makumira Tawi la Mbeya





muc2

CHUO KIKUU CHA TUMAINI MAKUMIRA - TAWI LA MBEYA
S L P 3040, MBEYA
TANGAZO LA NAFASI ZA MASOMO YA KOZI ZA UALIMU

Chuo Kikuu cha Tumaini Makumira Tawi la Mbeya ambacho awali kilijulikana kama Mbeya Lutheran Teachers’ College kinatangaza nafasi za masomo ya kozi ya Ualimu Ngazi ya Cheti,Stashahada na Shahada katika mwaka wa masomo 2013/2014.

1.    Sifa za Mwombaji
a)    Ngazi ya Cheti
                              i.        Mwombaji awe amefaulu mtihani wa kidato cha Nne kwa kiwango kisichopungua daraja la nne alama ishirini na saba (27) katika  mkao mmoja.
                             ii.        Awe amehitimu Elimu ya Sekondari  siyo zaidi ya miaka mitano iliyopita.

b)    Stashahada
                                      i.        Mwombaji awe na ufaulu wa principle moja na Subsidiary moja katika masomo yanayofundishwa Shule za Sekondari.          AU

Awe na Cheti cha daraja la tatu A chenye ufaulu wa wastani wa B au “Credit na Distinction”.   AU
Awe na cheti cha daraja la Tatu A na uzoefu usiopungua miaka mitano kazini.

Angalizo:Waombaji wote wanaotumia cheti cha Ualimu Daraja la Tatu A wanatakiwa kuwa na
ufaulu usiopungua “D” Tano katika mtihani wa kidato cha Nne.

c)    Kwa muombaji wa Shahada (Degree) tembelea tovuti ya TCU na chagua TUMA-MBEYA yenye code number MKM01 AU MKM02.

2.    Namna ya kutuma maombi.
(a)  Fomu za maombi zinapatikana katika Chuo Kikuu cha Tumaini Makumira tawi la Mbeya kilichopo Uyole. Au tembelea katika tovuti yetu www.shuco.ac.tz.
(b)  Mwombaji anatakiwa alipie Tshs. 30,000/= kama gharama za maombi katika akaunti namba:
ELCT-MLTC Computer Building Project (CRDB): 0152421083000
(c)  Barua iambatanishwe na Vivuli vya Vyeti vya kuhitimu Elimu ya Sekondari na Chuo.
(d)  Waombaji waliosoma Nje ya Nchi wawasilishe Vyeti vya Baraza la Mitihani la Tanzania ili vipatiwe utambulisho (kupasishwa).
(e)  Hati halisi ya malipo (Pay in Slip) iambatanishwe kwenye barua ya maombi.

3.    Muda wa mafunzo
Kozi ya Cheti na stashahada zitatolewa kwa muda wa miaka miwili na kwa kozi za shahada ni miaka mitatu.

KWA NGAZI YA CHETI NA STASHAHADA MASOMO YATAANZA RASMI TAREHE 08/07/2013

4.    Maombi yote yatumwe kwa
Mratibishaji wa masuala ya Taaluma
Chuo Kikuu Tumaini Makumira - Kituo cha Mbeya
S.L.P. 3040
MBEYA.
Simu no:  + 255 25 2510450
                  +255 0655 858 527/+255 753 817 274
Nukushi:  + 255 25 2510094
Tovuti: www.shuco.ac.tz
Barua pepe:   tumashuco2012@gmail.com




Wednesday, May 22, 2013

NATAMANI SANA

Natamani sana
Tamaa yangu ni kubwa
Kubwa kuliko niwezavyo sema
Kubwa sana hata siwezi maliza

Tazama watu wa mtwara
Wamepigwa mikwara
Wamepigwa mabomu
Kisa gesi 'yao'

Je ni yao
Yao peke yao
Iwafae wao
Kwa manufaa yao

Ni ya nani?
Je ya kiongozi nani?
Anamiliki nani?
Kwa manufaa ya nani?

Nachelea nisiwe miongoni mwao
Hao wawasemao
Wana wa Mtwara kuwa wamepoka gesi

Nisiwe miongoni mwa wanaolaumu
Eti mataifa ya nje yanaleta chokochoko,
Chokochoko tumeileta sisi
Kwa kutokujua haki za wazawa

Wanayo haki, haki ya kudai pato la gesi,
Wanayo haki ,haki ya kumiliki gesi
Hata kama sheria inasema madini ni ya UMMA,
Wao sio umma au umma wa nani?

Nani atasimama ataonesha usawa katika utajiri wa madini tuliobarikiwa nao
Nani atasimama atasema kuwa eti tumefaidika,,kwa kujengewa shule? Vyoo?
 Kwani TOFARI moja la DHAHABU lajenga VYOO, SHULE, ZAHANATI NGAPI?
Twahitaji MATOFARI mangapi ya TANZANITE ili tujenge barabara?

Wanayo haki,
Ya kutaka kuona namna watakavyofaidika,
Sio kuwapa ahadi
Zile za kwenye majukwaa.

Ifike mahali watu waoneshwe
Wapate kushika,
Hata Tomaso alikataa
Mpaka akatomasa

Vikionekana
Havibishiwi
Vikishikwa
Havikataliwi.

Pengine ni namna tu
Ya walivyodai
Wafanyeje
Kama mahakama ni sehemu ya dola

Wanayo kumbukumbu
Walimu walivyokomeshwa kugoma
Maana mahakama iligoma
Kuwaacha walimu wagome.

Wafanyeje,
WANA wa SIASA si wana WAO tena
Maana wao ni TAIFA teule
Lisiloguswa?

Wana wa SIASA,
Wana HISA
Wanafanya VISA
Utajiri waufaidi wao

Hawakuwa na namna nyingine
Pole wahanga wote
Hamtakwenda bure
Maana mfumo umewapoteza

Guebuza zamani alisema,,if we must die, let us die not like hogs
Hamjafa bure,
Mmefia 'a good cause',
Mungu awape subira, enyi wana wa MTWARA
Itapita hii MIKWARA,
MTASIKIWA.

Tamaa yangu ni kubwa
Kuona mali zetu twazifaidi
Sio kama KIWIRA COAL MINE
Mgodi umefungwa, Kisa ni nini? Waulize wana wa SIASA.

NATAMANI SANA,

WOTE KWA UMOJA TUGOME, TUDAI DHAHABU YETU, TWIGA WETU, NYATI WETU, FALU WETU, TANZANITE YETU, UTAIFA WETU,,,,NA MWISHO UTU WETU,,,


natamani sana,,,,

Tuesday, May 7, 2013

NANI AFANYE NINI?

Bibi yangu miaka ishirini iliyopita aliniambia maneno ambayo sijapata kuyasahau. Nilikuwa nimefadhaika sana ndipo katika mfadhaiko huo nikapata kutamka kitu ambacho kiliamsha hekima ya Marehemu bibi. Aliniambia 'ukiwa na furaha mwanangu (alizoea kuniita mwanae) usiahidi kitu, ukiwa na huzuni usitamke neno lolote na ukiwa na njaa usiahidi kitu'. Nimejitahidi sana kuishi katika hekima hii ingawa kuna muda huwa napotea maana ndio ubinadamu.
Nimeikumbuka hekima hii muda huu baada ya kusikia maana ilitangazwa kwenye redio na kusoma kwenye vyombo mbalimbali vya habari kuhusu mlipuko wa bomu (ingawa kuna baadhi ya TV zinaripoti kuwa kitu kinachohisiwa kuwa bomu! iwe vyovyote) uliotokea Arusha! Ni muendelezo tu wa yale yaliyotokea siku za nyuma, zilianza kama cheche, sasa zinakuwa si cheche tena! Nilitaraji mtu mmoja angezizima cheche hizi kwani moto hufa kwa kukosa kuni, lakini haijawa hivyo, bali nguvu nyingi zimeelekezwa kuzikataa cheche ambazo zinaongezeka.
Ndipo nikajiuliza niseme nini wakati huu wa fadhaa maana nachelea sana kumlaumu mtu, sasa nifanye nini? Je nikae kimya? Mpaka lini? ndipo nikasema nami niseme japo humu tu. Kwamba nitasikika sijui maana mimi ni mtu mdogo sana, tena sifahamiki kwa yoyote, laiti ningekuwepo mjengoni ningepaza sauti na kutunisha msuri pengine nikiunga mkono hoja,,,maana pasipo hivyo nitatukanwa nami sipendi matusi,,after all its about how much i make in the evening after a single sitting,,hadi raha kukaa tu hela,,,laiti wote tungekaa na kupata hela ingekuwa njema sana,,mmmh nisitoke kwenye hoja yangu ya msingi may be just may be siku moja nitasema umuhimu wa kukaa na kupata pesa,,maana iliandikwa zamani sana ,,KAENI NDANI YANGU,,,,,
Najiuliza nani afanye nini ndio swali langu. Ni kweli tumetikiswa na bomu, ni kweli Padri aliuwawa Zanzibar, je ni kweli vyombo vyetu TUKUKA havijaweza chunguza na kusokotoa nani kahusika? Je tumeshindwa kuwabaini hawa wabaya wanaotugawa sasa? Kuna udhaifu gani huo kupelekea kuwaomba FBI waje kwetu kuchunguza? Je wanachunguza hayo tu au na udhaifu wetu mwingine? Mbona tumeweza kwenda DRC na JESHI LETU TUKUKA? Tumeanguka wapi mpaka kuwaomba hawa FBI? Je yalipotokea mabomu kwenye MBIO za marathoni walituomba? ooh sorry they are better than us,,Je wataishia tu kuchungua bomu? Twahitaji sana kujua nani afanye nini wakati gani,,je si mwenye msiba aliaye sana kuliko waliokuja kuomboleza? Haya maadamu hatujiamini tena nachelea kusema hawa jamaa hawatatuacha mpaka wametuchunga oooh wametuchunguza na kutujua sana zaidi ya tujijuavyo,,mwisho wa siku tutawaomba wawe sungusungu wetu na ndipo tutawatumikia,,,,

Thursday, May 2, 2013

Hoja si meno ya Kinana tunaongelea meno ya TEMBO



Hoja si meno ya Kinana tunaongelea ya TEMBO


“Hoja ya Mzee Kinana hapa inakubalika kimantiki;
'Kampuni ni yangu, kila kitu ni changu ila meno si yangu'

NI KWELI MENO SI YAKE NI YA TEMBO! Lakini sasa huko kwenye kampuni yake huko yamefikaje? Na faida itokanayo na kazi inayofanywa na kampuni yake haiji kwake? Na hata mamlaka zinazopaswa kukagua meli si vya serikali ya chama anachokiongoza? Wanaposema serikali ya CCM in impotent, kwanini asikubali tu?” Fuatilia mjadala huu kwenye facebook http://www.facebook.com/photo.php?fbid=10201162411003067&set=a.1455905638322.64825.1253767086&type=1&theater&notif_t=photo_comment

SUBSCRIBE- Andika email yako hapa utumiwe habari mpya

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008 modified by Subi nukta77

Go Back to TOP