Pekua/search

Saturday, April 12, 2008

Mama Salma Kikwete aigwe.

Tangu alipoingia madarakani, Rais wa awamu ya nne Jakaya Kikwete, mkewe, first Lady Salma amekuwa mstari wa mbele katika harakati mbalimbali. Harakati zake hizo zimehusisha kukaribisha wageni wengi mbali mbali kutoka mataifa ya karibu na mbali.

Mara nyingi, kama si zote, mama Salma amekuwa akitumia Kiswahili katika hotuba zake kwa wageni wake.Hapa ndipo ninapompongeza mama huyu. Mwanzoni wengi wetu tulidhani ni kutokana na yeye kutokuwa bingwa katika lugha ya Kiingereza, lakini nadhani mpaka sasa tumejihakikishia kwamba tulichemka. Mama huyu Mwalimu kitaaluma na kitaalamu, anakijua Kiingereza vizuri kabisa.

Mrengo aliouchukua mama Salma nadhani ni wa maksudi kabisa. Ameamua kuwa Mtanzania anayejivunia Kiswahili. Na kwa hili, amekuwa mfano hata kwa mumewe, Rais wetu JK ambaye naweza kusema anakionea aibu Kiswahili. Mfano mzuri wa kuthibitisha hoja hii, ni pale alipoangushwa na Kibaki na Odinga huko Nairobi, siku si nyingi zilizopita. Baada ya kufanikiwa kuwaweka pamoja ndugu hao wa Kenya, rais Kikwete kwa nafasi yake akiwa kiongozi mkuu wa Umoja wa Afrika, alitoa hotuba yake kwa Kiingereza (Kiongozi wa Kwanza kuhutubia AU kwa Kiswahili alikuwa Chisano wa Msumbiji). Mkapa hakuwa na ujasiri huo!!

Rais wa Tanzania anatoa hotuba kwa Kiingereza katika eneo la Afrika Mashariki, nani abebe bendera ya Kiswahili duniani? Tofauti na kiongozi huyo wa Au, 'faraja' ikaja pale Raila Odinga na Mwai Kibaki walipohutubia kwa Kiswahili. ndipo ninaposema 'walimwangusha JK' hawa Wakenya.

Mwelekeo wa mama Salma hauna budi kuigwa na kuungwa mkono na Viongozi wetu wa Kitanzania. Tunafahamu wanajua Kiingereza vizuri. Lakini wanalo jukumu la kukienzi Kiswahili. Wanalojukumu la Kukieneza na kukitangaza Kiswahili. Wanalo jukumu la kututafutia kazi za ukalimani sisi vijana wa kitanzania kwa wao kuzungumza Kiswahili bila aibu.TUNAWATEGEMEA.WAMECHELEWA SANA.

Ni mara nyingi viongozi wetu wametumia Kiingereza pasipo hata na ulazima wa kufanya hivyo. Inafahamika wazi mathalan, kwamba Rais wetu akienda na ujumbe wake Uingereza, hawezi kuwafanya viongozi wa nchi hiyo wazungumze Kiswahili. Vivyo hivyo akienda Uchina na Japani, watazungumza lugha zao viongozi wa nchini hizo, na ujumbe wa Tanzania utawasiliana na wenyeji wao kupitia Wakalimani na Wafasiri. hiki ndicho alichokianzisha mama Salma. Anakimwaga Kiswahili mtoto wa Kitanzania.Wageni wake wanapata fursa ya kuuonja utamu wa lugha hii adhimu.

HONGERA MAMA SALMA. ENDELEA. KANYAGA TWENDE, HAKUNA KURUDI NYUMA. MJENGA NCHI NI MWANANCHI MWENYEWE.

Pengine wakati umefika kwa viongozi wengine kukienzi Kiswahili kwa kukitumia, hususan katika hotuba zao ndani ya nchi. Bungeni ndiyo kabisaaaa.

Mungu kibariki Kiswahili. Mungu Ibariki Tanzania.

Adam, L

0 comments:

SUBSCRIBE- Andika email yako hapa utumiwe habari mpya

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008 modified by Subi nukta77

Go Back to TOP