MCHAKATO WA JK WA KUTENGANISHA UONGOZI NA BIASHARA UMEFIKIA HATUA GANI?
Mojawapo ya Hotuba za Rais wetu Jakaya Kikwete iliyonigusa ni ile aliyozungumzia suala la kutenganisha Uongozi na Biashara. Soma hapo chini sehemu ya hotuba hiyo. Hata hivyo sentensi hii yaweza kuwa muhimu zaidi pengine (way forward),
"Kwa ajili hiyo ni makusudio yangu kuanzisha mchakato wa kufanya marekebisho ya Sheria ya Maadili ya Uongozi ili tuingize utaratibu huo." alisema Mhe. Rais.
Ni zaidi ya amwaka mmoja na nusu sasa; Je mchakato umeshaanza na Umefikia hatua gani? Tafadhali mliona taarifa tushirikisheni. Nini kilimsukuma rais kusema maneno haya kwa kishindo? Je yaweza kuwa kweli kwamba HOFU YA RIPOTI KUHUSU RICHMOND Ilichangia kumfanya rais wetu akimbilie kusema hivyo kama njia ya kuwakoa baadhi ya 'jamaa zake' ambao wangeweza kuwahusishwa na kashfa ya Rchmond? Na kwamba baada ya sakata la Richmond kuisha au kuendelea kuisha kama hali ilivyojitokeza, rais wetu akakosa nguvu na msukumo wa kuendeleza au hata kuanzisha mchakato? Kama kweli hajauanzisha basi ndugu mliokwenye nafasi ya kumkumbusha, HEBU MKUBUSHENI JAMANI, walau hili likitendeka, tutakuwa tumemuenzi Baba wa Taifa na Azimio 'lake' la Arusha na maudhui ya kimaadili yaliyokuwemo.
Soma sehemu ya hotuba ya Rais kwa wananchi, 31 Januari, 2008.
"Tutenganishe Uongozi na Biashara
Ndugu Wananchi;
Jambo la mwisho ninalotaka kulizungumzia linahusu maadili ya uongozi nchini. Hususan napenda kulizungumzia suala la viongozi wa siasa Mawaziri na Wabunge kuwa pia watu wanaojihusisha na shughuli za biashara moja kwa moja. Upo ushahidi wa kuwepo migongano ya maslahi kwa baadhi. Lakini, pia, hata pale ambapo hakuna dalili za wazi, hisia za kupata manufaa yanayotokana na nafasi zao hutawala. Matokeo ya yote hayo ni watu kupoteza imani na kutilia shaka uadilifu wa viongozi wetu.
Ndugu Wananchi;
Nchi za wenzetu hasa zile za kibepari zinazo taratibu nzuri za kushughulikia hali hizo. Wenzetu wanao utaratibu unaomtaka mtu mwenye shughuli za kibiashara anapokuwa Mbunge au Waziri kuacha kujishughulisha na biashara zake. Unakuwepo utaratibu rasmi unaotambuliwa kisheria wa wadhamini wanaoendesha hizo shughuli bila ya yeye kujihusisha nazo. Anapoacha uongozi wa siasa kama atapenda atachukua tena mali yake na kuendelea na shughuli zake.
Ni makusudio yangu kuwa utaratibu huu tuuanzishe hapa nchini. Viongozi wetu wachague kufanya jambo moja kwa wakati mmoja ama biashara au Ubunge na Uwaziri. Kwa ajili hiyo ni makusudio yangu kuanzisha mchakato wa kufanya marekebisho ya Sheria ya Maadili ya Uongozi ili tuingize utaratibu huo.
Ndugu Wananchi;
Ni jambo lenye maslahi kwa nchi yetu na litasaidia sana kujenga heshima ya viongozi wa umma mbele ya macho ya wananchi. Nafurahi kwamba suala hili tumelizungumza katika kikao maalum cha Kamati Kuu ya CCM tulichofanya Dodoma juzi tarehe 29 Januari, 2008 na tumeelewana. Ni matumaini yangu kuwa sote tutaunga mkono.
Mwisho, nawatakia kila la heri kwenye shughuli zenu. Tuendelee kushirikiana kuijenga na kuiendeleza nchi yetu. Asanteni sana kwa kunisikiliza."