Pekua/search

Thursday, July 25, 2013

Serikali Tatu Zitapunguza Gharama za Uendeshaji



Serikali Tatu Zitapunguza Gharama za Uendeshaji

 Gharama za ziada zinaweza kuepukwa mathalan kwa kuiondosha Ofisi ya Makamu wa Rais na kuivunjilia mbali ofisi ya Waziri Mkuu butu asiye na meno hata kucha

Kinachoelekea kuuteka mjadala wa katiba mpya hivi sasa ni pendekezo la serikali tatu. Naunga mkono serikali tatu kwa kuwa kiuhalisia imethibitika kuwa vigumu kuwa na serikali moja kwa kisingizio cha kumezana. Na hizi mbili zimechusha kero zake na viraka vimekuwa vingi mno kiasi kwamba nguo yetu hii Muungano itatatuka pasipo kujitafakari upya.

Sababu kubwa inayoonekana kuwa nzito ni kuhusu gharama. Ninachangia hili la gharama kwenye makala hii fupi.

 Serikali tatu zinaweza kuokoa sana gharama ikiwa tutaacha hofu ya kisichojulikana na kujikita katika kufikiri kwa kutumia mbongo na sio visigino nk kama walivyofanya kina Nyerere na Karume walivyofikiri kwa mbongo zao na nia na dhati ya mioyo kabisa. Nasi sasa tunao wajibu; Tukiutimiza wajibu huu tutatuzwa na tukiutelekeza tutatwezwa maana ilishanenwa Likulli ajalin kitab', yaani kila zama ina kitabu chake,”

Gharama za ziada zinaweza kuepukwa mathalan kwa kuiondosha Ofisi ya Makamu wa Rais na kuivunjilia mbali ofisi ya Waziri Mkuu butu asiye na meno hata kucha (ofisi na sio mhe Pinda). Viongozi wakuu wa serikali hizi mbili yaani  Tanzania Bara na Zanzibar  ndiyo watakuwa wasaidizi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na mawaziri wachache wa kisekta watakuwa wasaidizi wa karibu wa viongozi wakuu wa serikali hizi mbili za Tanzania bara na Zanzibar .

Bajeti inayotumika sasa kuendesha ofisi ya Rais itatumika kuendesha ofisi ya Rais wa Muungano sambamba na kusimamia masuala ya Muungano. Gharama za uendeshaji wa ofisi ya Waziri Mkuu na sehemu ya bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Rais sasa zitatumika kuendesha Ofisi ya Kiongozi wa Serikali ya Tanzania Bara (bila kujali cheo cha kiongozi huyo ataitwaje). Bajeti za wizara ambazo si za muungano (hizo zipo hata sasa) hata hivyo zinaweza kupunguzwa.

Gharama za uendeshaji wa serikali ya Zanzibar wala haina haja hata kuhofia maana hizo zipo hata sasa.

Ni gharama zipi tunazozihofia kuongezeka katika kuendesha serikali tatu?

Kwa upande wa Bunge
Bunge la Muungano halitakuwa na haja ya kukaa muda mrefu kama ilivyo sasa kwani masuala ya muungano si mengi kiasi hicho. Gharama za muda utakaookolewa zitatumika kuendesha bunge la Bara. Hali kadhalika Bunge la Tanzania Bara litapungua ukubwa wake na hivyo kupunguza gharama tofauti na hivi sasa ambapo wakati wa kujadili masuala ya bara yasiyo ya muungano wabunge kutoka zanzibar huwa hawatoki wanakuwepo na posho wanalamba kama kawaida ilhali mijadala inayoendelea inahusu mambo ‘yasiyowahusu’.

Gharama gani tunazihofia? Mambo yasiyo ya Muungano kwa upande wa Visiwani yanajadiliwa na baraza la wawakili hata sasa. Serikali tatu zinaweza kupunguza gharama hata zile za vikao vya mapatano na kutanzua kero za muungano wa serikali mbili za sasa ambazo hazitanzukiki.

SUBSCRIBE- Andika email yako hapa utumiwe habari mpya

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008 modified by Subi nukta77

Go Back to TOP