Pekua/search

Monday, October 25, 2010

Mambo 10 unayotakiwa kujua kuhusu Kura yako

Mambo 10 unayotakiwa kujua kuhusu Kura yako

by Mimi Mwanakijiji on Tuesday, October 26, 2010 at 5:29am
MAMBO AMBAYO UNATAKIWA KUJUA KUHUSU KURA YAKO:Na. M. M. Mwanakijiji

Kura yako ina nguvu gani na kwanini?

1. Kura yako ndiyo lugha pekee ambayo wanasiasa wanaielewa. Wanasiasa wote duniani wanaweza kuwa wabishi na wenye kelele sana lakini ni kura tu ndiyo inaweza kuwalazimisha kusikiliza. Kama unataka kumwambia mwanasiasa akusikie? Piga kura!

2. Kura yako ni silaha pekee katika demokrasia ya kuwaadhibu wanasiasa wabovu na viongozi uchwara. Katika demokrasia wananchi waliochoshwa hawahitaji bunduki wala mapanga kuonesha hasira yao, wanahitaji karatasi ya kura na kutoa kipigo chao kwenye sanduku la kura! Ndio maana tunaita “kupiga kura”!

3. Kura yako ni siri yako. Hakuna mtu anajua umepigaje au utapigaje kura hata kama anajua wewe ni mwanachama wa chama gani. Kama siri nyingine za mioyo njia pekee ya mtu mwingine kujua ulivyopiga kura ni kwa wewe kumwambia, usipomwambia hawezi kujua. Hakuna Polisi, Idara au chombo chochote cha usalama kinaweza kujua ulivyopiga kura! - Piga Kura

4. Kura yako ndio utekelezaji wa uamuzi wako. Mtu kabla hajapiga kura ni lazima afanye uamuzi kwanza ni mgombea gani anamtaka na kwanini na akishafikia uamuzi huo basi anaingia kwenye chumba cha kupigia kura na kuutekeleza uamuzi huo. Bila kupima uamuzi wako utapata shida kupiga kura, amua kwanza, halafu piga kura!

5. Kura yako si deni kwa mtu au chama chochote. Pamoja na kuwashangilia wagombea au kuonesha kupendezwa na hoja zao hayo yote hayakufanyi ujihisi unadaiwa nao. Kura ni haki yako wewe siyo haki yao wao. Hivyo, una haki ya kumpa mtu yeyote kura hata kama si wa chama chako bila kujisikia umemnyima mtu haki yake. Kura ni haki yako wewe!

6. Kura yako yaweza kwenda kwa mtu yeyote au chama chochote bila kukufanya ujisikie umsaliti. Utakapoingia kwenye chumba cha kura una haki ya kubadilisha kura yako kwa kadiri ya dhamira yako. Ukiwa na wasiwasi kuhusu kumpigia kura mtu hasa unayemtaka kwa kuogopa kuwa wanaweza kukujua soma namba  (3). Piga kura kwa kufuata dhamira!

7. Kura yako ina matokeo kwa vizazi vijavyo siyo kwa leo tu. Usipige kura kwa kuangalia furaha ya leo au kukidhi mahitaji ya leo tu, kura utakayopiga itaamua nani apange mipango na kusimamia mipango kwa miaka mitano ijayo na mingine inayoweza kuvuka vizazi. Hivyo, usipige kura kwa kuridhisha hisia za leo, fikiria kizazi kijacho kitanufaika na uamuzi wako?

8. Kura yako inapoombwa na wagombea wanachogombea ni ajira kutoka kwako. Wewe ndiye muajiri wa wanasiasa wote kuanzia Rais hadi diwani. Hawana haki na kura yako kama vile mfanyakazi hana haki na mali ya bwana wake. Ndio maana wanapita kuomba kura yaani ajira. Ni lazima ujiulize je kama mtu anaoomba kibarua kwako utampa tu bila kuangalia kama ataweza kufanya kazi na unaweza umuamini? Hivyo, baada ya kuwasikiliza waomba kazi waliopiga kila sehemu je uko tayari kuwaajiri wakufanyie kazi ya kuliongoza taifa lako?

9. Kura yako ndiyo huduma zote za jamii unazozitaka. Kwa vile kura yako ndiyo inaamua nani anaingia madarakani na kupanga nini na kutekeleza vipi basi kura yako ndiyo itaamua watoto wako watasoma katika shule gani, mfumo wa utawala utakuwaje, jeshi la polisi linafanyaje kazi n.k Hivyo, kura yako ndiyo barabara, maji, elimu, utawala, n.k Piga kura ukijua unataka upatiwe nini na nani?

10. Kura yako ni dhamiri yako. Kila mwanadamu anayo dhamira ndani yake yaani ile sauti ya ndani inayotufanya tukatae vitu vibaya na kuvipenda vizuri, ile sauti inayotuonya tunapofanya vibaya na kutupongeza tunapofanya vizuri. Ni ile sauti ya kimya ndani ya mioyo yetu inasimama kama shahidi wa maamuzi na matendo yetu. Dhamiri hii katika siasa inaoneshwa katika kupiga kura. Unapoenda kupiga kura hakikisha umepima mambo yote yanahuusu wagombea na ajenda zao na mwisho fuata dhamira yako. Usipoisikiliza dhamiri yako utaishi na majuto, usiishi na majuto!

Hivyo basi, tumia haki yako ya kupiga kura kumchagua mgombea ambaye unajua atafaa kuliongoza taifa kwa miaka mitano ijayo. USIOGOPE, USIBABAISHWE NA KAMWE USITISHWE ATI USIPIGE KURA! Weka miadi na historia, piga kura!

ORODHA YA AHADI ZA WAGOMBEA 2010; NANI ZAIDI?


Nani katoa ahadi nyingi zaidi? zipi zitatekelezeka? Nani mwenye uwezo wa kutekeleza ahadi hizi?

My take: nyingine ni za kijumla jumla mno; ni ngumu kupima utekelezaji wake. Ahsante:

 
Dk. Mohammed Shein (CCM)
  1. Kuboresha maisha ya wavuvi-Chakechake Pemba
  2. Kusomesha wafanyakazi-Mnazi mmoja
  3. Kipaumbele katika elimu -Unguja na Pemba
  4. Kipaumbele katika afya-Makombeni Mkoa wa Kusini Pemba.
  5. Kuulinda Muungano- Wawi kisiwani Pemba
  6. Kuleta mabadiliko Zanzibar-Pemba na Unguja
  7. Kuboresha Bandari ya Zanzibar kwa kuijenga upya-Kibandamaiti
  8. Kuboresha Maendeleo Zanzibar- Jimbo la Wete, Pemba
  9. Ujenzi wa maktaba kubwa na nzuri Kisiwani Pemba- Mtambwe
  10. Kutokomeza ugonjwa wa kipindupindu Zanzibar- Kijiji cha Kambini Mchangamdogo
  11. Kuimarisha miundombinu Kisiwa cha Pemba- Kijiji cha Makombeni Mkoa wa Kusini Pemba
  12. Kuhamasisha wawekezaji kuwekeza Pemba katika miradi mbalimbali-Makombeni Mkoa wa Kusini Pemba.
  13. Ahadi eneo la Micheweni kuwa maeneo huru ya uchumi- Micheweni Kaskakzini Pemba
  14. Kumaliza matatizo ya maji mkoani -Mkoani
  15. Kujenga Bandari ya kisasa katika eneo la Mpiga Duri Unguja- Mkoani
  16. Kuiamrisha makazi bora kwa Wazanzibar- Mkoani

Dk. Slaa (CHADEMA)

  1. Kujenga nchi isiyo na ufisadi
  2. Kufufua Tanganyika ili irejee mezani kujadili muungano na Zanzibar
  3. Kufufua uchumi wa nchi kwa kutumia rasilimali zilizopo
  4. Kukata asilimia 20 ya mshahara wa rais5.Kupunguza mishahara ya wabunge kwa asilimia 15
  5. Kuweka Mwenge wa Uhuru Jumba la Makumbusho
  6. Kutoa huduma bora za afya bure
  7. kufuta kodi ya vifaa vya ujenzi
  8. Kuwalipa wazee wa EAC fedha zao ndani ya siku 100
  9. Kubana matuzi Ikula (Yuko tayari kula mihogo)
  10. Elimu bure kuanzia Chekechea hadi Kidato cha Sita
  11. Katiba mpya ndani ya miaka mitano

Profesa Lipumba na Maalim Seif (CUF)

  1. Elimu ya bure kuanzia msingi hadi chuo kikuu
  2. Kubana matumizi kwa kupunguza ukubwa wa baraza la mawaziri
  3. Kuunda Serikali shirikishi
  4. Kusimamia rasilimali
  5. Kuimarisha miundombinu
  6. Kusimamia na kuboresha afya
  7. Kuboresha kilimo, viwanda na uwekezaji
  8. Kurudisha chakula cha bure mahospitalini

Maalim Seif (CUF)

  1. Zanzibar kuwa kama Hong Kong – Unguja
  2. Kuendeleza mashamba ya Karume- Kibanda maiti
  3. Kubadilisha katiba na kuunda katiba mpya ya muungano na Zanzibar- Pemba
  4. Kubadilisha mfumo wa uteuzi makamishna wa tume ya uchaguzi Zanzibar (ZEC)- Unguja
  5. Kuwaunganisha Wazanzibari ili kujenga umoja, udugu na ushirikiano-Pemba
  6. Kuwasilisha hoja ya kubadili katiba ya Zanzibar na ya Muungano-Viwanja vya Kibanda Maiti
  7. Kuondoa bajeti ya ZEC isiwe chini ya waziri kiongozi na badala yake kuwa inajitegemea yenyewe- Pemba
  8. Kuondoa ulazima wa mwenyekiti wa tume kuwa jaji na badala yake awe mtu anayejua sheria-Unguja
  9. Serikali kuundwa na vyama vyote vilivyopata ridhaa ya kuchaguliwa na wananchi- Unguja
  10. Kujenga jamii yenye maelewano na umoja -Pemba
  11. Kutokochagua kiongozi kwa urafiki bali kwa uwajibikaji na uadilifu -Unguja na Pemba
  12. Kudhibiti vyombo vya dola vinavyofanya kazi kwa matakwa ya watu binafsi -Kibanda aiti
  13. Kukomesha rushwa-Mkanyageni Mkoa wa Kusini Pemba
  14. Kuhakikisha ununuzi wa zabuni unakuwa wazi na wananchi kuruhusiwa kuhoji kuhusu zabuni-Jimbo la Dole Pemba
  15. Kuongeza kima cha chini cha mshahara hadi Sh150,000-Mkanyageni Pemba
  16. Kubadili vikosi vyote vya usalama na kulipwa mishahara kima cha chini kulipwa Sh 180,000-Chakechake Pemba
  17. Kubadilisha kikosi cha KMKM kuwa kikosi cha mwambao-Wawi
  18. Wazee kupanda daladala bure na wale wasiokuwa na watoto kulelewa bure-Majimbo ya Chakechake
  19. Kufuta michango yote ya shule za msingi na sekondari, kila mwanafunzi kuwa na kompyuta na badala ya kuishia darasa la saba sasa kuishia kidato cha sita-Hoteli ya Bwawani
  20. Kutoa kitambulisho cha kila Uzanzibari na kufuta cha Mzanzibari mkaazi- Uwanja wa Hospitali ya Mnazi Mmoja
  21. Kila Mzanzibari kupata pasi ya kusafiria- Hoteli ya bwawani Zanzibar
  22. Kuanzisha shirika la ndege Zanzibar -Viwanja vya Kibanda Maiti
  23. Kupandisha uchumi wa Zanzibar kutoka 6.8 hadi 15 kila mwaka kwa Zanzibar -Unguja
  24. Kutoa uhuru zaidi kwa vyombo vya habari pamoja na kusaidia uanzishwaji wa Baraza la Habari Zanzibar-Unguja na Pemba
  25. Kuweka hadharani nambari yake ya simu - Viwanja vya Kibanda Maiti
  26. Kubadili sheria ya uwekezwaji-Hospitali ya Mnazi Mmoja Zanzibar
  27. Kila mwanafunzi kuwa na komputa yake-Viwanja vya Kibanda Maiti
  28. Akiwa rais hata waziri au mkewe atafungwa akiwa ametenda kosa-Viwanja vya Tibirizi Kisiwani Pemba
  29. Kujenga bandari ya Mkokoto na Pemba ili kuweka usafiri wa haraka wa boti ziendazo kasi-Tibirizi Kisiwani Pemba
  30. Ahadi kudhibiti kuvuja kwa mitihani- Unguja

Kikwete (CCM)

  1. Kujenga reli mpya kutoka Dar es Salaam mpaka mikoa ya Kanda ya ziwa-Nzega, Tabora
  2. Mkoa wa Tanga kuwa Jiji la Viwanda- Tanga mjini
  3. Tabora kutumia maji ya Ziwa Victoria-Igunga
  4. Kulipa madeni ya chama cha Ushirika mkoa wa Shinyanga (SHIRECU)- Shinyanga
  5. Kumaliza migogoro ya Ardhi nchini- Dodoma
  6. Wakulima kuacha kutumia jembe la mkono-Dodoma mjini
  7. Kuwapatia trekta wakulima -Kata ya Mrijo, Dodoma
  8. Wananchi kutoondolewa kwenye Ranchi ya Misenyi-Kagera
  9. Kujenga Uwanja wa Ndege Misenyi-Kagera
  10. Kupanua Uwanja wa Ndege Bukoba-Bukoba Mjini
  11. Kujenga uwanja wa ndege mkubwa Kigoma - Kigoma Mjini
  12. Mtukula kupatiwa umeme kutoka Uganda- Kagera
  13. Mikoa ya Kagera, Kigoma, Lindi, Rukwa na Ruvuma kuunganishwa katika gridi ya taifa ya umeme- Kagera
  14. Kuimarisha Takukuru kwa miaka mitatu-Kagera
  15. Hukumu kwa waliopatikana na hatia ya kuua albino- Mbeya
  16. Kununua meli kubwa kuliko MV Bukoba-Kagera
  17. Kuanzisha benki ndogondogo kwa ajili ya wajasiriamali
  18. Serikali kuvisaidia vyama vya ushirika-Mwanza
  19. Kuimarisha usalama Ziwa Victoria na Ziwa Tanganyika kwa kupeleka kikosi maalum chenye vifaa kupambana na wahalifu-Mwanza
  20. Wilaya ya Geita kuwa hadhi ya mkoa Januari mwakani- Geita
  21. Kulinda Muungano kwa nguvu zote-Pemba
  22. Kuwajengea nyumba waathirika wa mafuriko Kilosa-Morogoro
  23. Kununua meli mpya kubwa Ziwa Nyasa-Mbeya mjini
  24. Kujenga bandari Kasanga –Rukwa
  25. Kumaliza tatizo la walimu miaka mitano ijayo - Songea
  26. Kufufua mgodi wa makaa ya mawe Kiwira -Mbeya
  27. Kuzuia hatari ya kisiwa cha Pangani kuzama- Tanga
  28. Kununua "bajaji" 400 kwa ajili ya kubeba wajawazito hasa vijijini- Iringa
  29. Kujenga barabara yenye kiwango cha lami kutoka Same mpaka Kisiwani –Kihurio na kuiunganisha na barabara kuu ya Moshi -Dar es salaam- Same mkoani Kilimanjaro
  30. Kumaliza tatizo la maji katika wilaya ya Same-Same Mjini
  31. Kuboresha barabara za Igunga -Tabora
  32. Kusambaza walimu 16,000 katika shule za Sekondari zenye upungufu makubwa wa walimu- Kisesa Magu
  33. Kununua vyandarua viwili kwa kila kaya- Mbeya Mjini
  34. Kuzipandisha hadhi hospitali maalumu saba nchini kuwa za rufaa ili kuipunguzia mzigo Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MHN)-Hydom Manyara
  35. Kulinda amani nchini kwa kuzuia chokochoko za kidini, kikabila na kisiasa- Musoma
  36. Kulinda haki za walemavu- Makete
  37. Kujenga baabara ya Njombe- Makete kwa kiwango cha lami,urefu wa kilomita 109- Iringa mjini
  38. Kujenga barabara Musoma–Mto wa Mbu Arusha-Arusha
  39. Kuanzisha jimbo la Ulyankulu- Shinyanga Mjini
  40. Kujenga barabara ya lami Manyoni-Kigoma– Kaliua,Tabora
  41. Kukarabati barabara ya Arusha Moshi-Arusha Mjini
  42. Kuboresha barabara ya Handeni, Kondoa mpaka Singida-Dodoma
  43. Kuwafidia wanakijiji ng’ombe waliopotea wakati wa ukame mwaka 2009- Longido 45.Vijiji vyote vilivyoko kilomita 15 kutoka kwenye bomba kuu la mradi mkuu wa maji wa Ziwa Victoria-Shinyanga-Kahama kuunganishiwa maji - Shinyanga
  44. Tatizo la umeme kufikia kikomo Novemba mwaka huu mkoani Arusha –Arusha mjini
  45. Kukopesha wavuvi zana za kilimo-Busekera, Wilaya ya Musoma, .
  46. Kuwapatia maji wakazi wa Wilaya ya Longido- Longido
  47. Kujenga barabara ya lami kupitia pembezoni mwa Hifadhi ya Taifa ya Seregenti – Ngorongoro
  48. Utekelezaji wa mpango wa maendeleo ya kilimo kuwasaidia wafugaji kuweza kupata na kutunza mifugo yao vizuri- Mbulu mkoani Manyara
  49. Kusambaza maji nchi nzima-Babati vijijini
  50. Kusambaza umeme, utoaji wa huduma za afya, na uboreshaji wa kilimo cha umwagiliaji na utoaji ruzuku kwa wakulima. mwaka 2010-2015-Babati vijijini Kuongeza mara tatu idadi ya wananchi wanaonufaika na ruzuku ya pembejeo za kilimo kwa mfumo wa vocha.-Iringa
  51. Kuhakikisha Isimani inapata maji ya uhakika- Iringa
  52. Kuiwekea lami barabara inayokwenda katika Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, ambayo ndiyo hifadhi kubwa kuliko zote Tanzania-Iringa
  53. Kulinda usalama wa wananchi kwa ujumla ili kudumisha amani na sifa ya nchi-Ifunda
  54. Kutokomeza malaria 2015-Bunda, Mkoa wa Mara
  55. Kuwapa wanawake nafasi zaidi-Kilolo, Iringa
  56. ahadi kuisadia Zanzibar kuendeleza miradi mbalimbali ya kijamii-Kibandamaiti Mjini Zanzibar
  57. Kuipandisha hadhi hospitali ya Mnazi Mmoja Zanzibar kuwa ya rufaa-Kabandamaiti mjini Zanzibar
  58. Kuisaidia Zanzibar kila panapohitajika msaada-Kibandamaiti
  59. Serikali kujenga upya bandari ya Mbambabay-Ruvuma
  60. Ununuzi wa Meli mpya yenye uwezo wa kubeba tani 400 - Mbamba-bay Ruvuma
  61. kufufua chama kikuu cha ushirika cha wakulima wa Mbinga (MBICU) –Ruvuma
  62. Ahadi Rais wa Marekani Barack Obama kuimwagia misaada Tanzania –Ruvuma
  63. Ahadi hakutakuwa na umwagaji wa damu baada ya uchaguzi-Dar es Salaam
  64. Mtwara kuwa mji wa Viwanda –Mtwara
  65. Ahadi ujenzi wa kwanda cha dawa ya kuua viluilui vya mbu-Kibaha
  66. Hospitali ya Tumbi kuwa ya mkoa-Kibaha
  67. Halmashauri ya manispaa ya Kibaha kutenga eneo maalumu la viwanda -Kibaha
CHANZO tovuti ya Wavuti hapa (wavuti.com ) awali iliandaliwa na mwandishi wa habari, bwana Francis Godwin na ameorodhesha katika toleo alilolichapisha kwenye blogu yake hapo tarehe 22 Oktoba 2010.

Tuesday, October 12, 2010

MACHOZI NDANI YA DALADALA - NI NZURI KUSOMA

Ni habari ya siku kidogo, lakini yafaa kusomwa na mbayuwayu wengi zaidi. Nimeipata HAPA



Nikiwa kati ya WATU waliohudhuria mikutano ya kampeni hasa ya urais,nimeona mengi,nimesikia mengi,ahadi kemkem,tam,nzuri na zenye kuvutia na kama JK,SLAA au LIPUMBA mmoja wo akishinda na kutekeleza ahadi zake basi TANZANIA itakuwa kama Boswana au kama sio kuifikia Afica kusini. Sina sababu ya kuzitaja ahadi kwani wengi wenu mwazijua.

    Ni saa 12:30 za jioni siku ya ijumaa,natoka ofisini kwangu JMOO nakwenda posta ili kupanda gari la kuelekea mbezi nyumbani kwangu(mbezi ya kimara).Abiria ni wengi kama kawaida,wezi wamo,ila kuna magari ya kwenda mbezi ya buku(elfu moja) naingia na muda si mrefu gari inajaa na kuondoka,wote tumekaa,foleni ni kama kawaida kwani inaanzia faya na uku gari ikiwa imewekwa radio moja ya chama tawala.Watu tupo kimya na aliyesimama ni konda tu.

    Mara hiyo radio ikaanza kutangaza sera za mgombea uras wa chama tawala,ahadi nyingi,kile mara iki najua mwazijua sina shida ya kuzitaja ila ni moja tu ambayo nitaitaja ambayo imenipelekea kuandika UJUMBE huu kwenu,ni ile ya KUNUNUA BAJAJI 40 KWA WAMAMA WAJAWAZITO,hapo ni saa 1:30 za jioni na hatujavuka magomeni.

    Mara baada ya huyo mgombea kutaja iyo ahadi,nikasikia sauti kuoka nyuma ya gari ikisema “ZIMA RADIO YAKO AU BADILISHA STESHENI”ni sauti ya kike tena mwanamama mjamzito.Dereva alizima radio,tukawa kimya kila mtu nahisi alikuwa anajiuliza kwanini huyu mama kasema radio izimwe au ibadilishe stesheni,ukimya ulitawala kama dk 15.Tukiwa tunaanza foleni ya ubungo pale mahakama ya ndizi au bigbrother, na ikiwa ni saa 2:07 za usiku,nikasikia sauti ya mwanamama mwingine(sio mjamzito) ikisema “KAMA MIMBA ZINGEKUWA ZINABEBWA KWA ZAM HUYU KIKWETE ASINGETAMKA MANENO HAYO”nikashtuka nikageuka nyuma nikakutana uso kwa uso na yule mama mwenye mimba,mimba yake ilikuwa ni kama ya miezi nane tena ilikuwa kubwa(namaanisha tumbo ni kubwa sana).

    Tukiwa tupo stand ya mkoa na gari likiwa limesimama na ni saa 2:45 usiku kumbuka nimetoka posta saa 12:30 za jioni.Yule mama mjamzito akasimama akaanza kusema “MIMI SITOMPA KURA KIKWETE KWA JAMBO ILI,NILIKUWA NIMPE ILA KWA JAMBO KAMA ILI SIWEZI KUMPA”uku akilia na kutokwa na machozi,yule mama mwingine aliyesema “kama mimba zingekuwa zinabebwa kwa zam huyu kikwete asingetamka maneno hayo” akaanza kumbembeleza yule mama mjamzito akimsii akae.Nilimtazama kila mtu ndani ya gari sura zilibadilika zikawa sura za majonzi.

    Nikatoka kwenye daladala(kimawazo) nikaleta taswila ya BAJAJI nikamuweka yule mama nyuma na mimi nikawa dereva,nikafikiria umbali wa kilometa 50 toka kijijini kwetu kule kanyigo kuja hospital,barabara imejaa mashimo,nikawaza tumbo la yule mama akiwa yuma na uchungu na babaji ikiwa inayumba kwenye mabonde ya barabara,”NILILIA” nilishutushwa na honi nyingi za magari ambazo zilikuwa zikilipigia daladal letu kwa kutotembea, kwani kila mtu alikuwa kwenye mawazo ya yule mama(naisi) na dereva alijisahau kwa kumuonea huruma yule mama.Nilikuwa karibu na dereva nikamuuliza vp?,akajibu “WE ACHA TU”uku akitoa leso na kufuta machozi na kuanza kuendesha gari.

    Ni saa 3:07 usiku tupo kimara tunaanza foleni ya kimara stopover,watu wote wapo kimya akuna aliyeshuka mpaka sasa na konda kaka kwenye mlango ameinama,kila mtu kainama,uku wengine wakivuta mafua,na yule mama mjamzito akionekana ana asira na uku machozi yakimtoka yenyewe.Nikajiuliza ina maana watu wote tunakwenda mbezi?,pia huyu mama vp mbona kabadilisha kila mtu ndani ya daladala? Katumwa nini?.Nikasikia sauti ya baba mmoja kutoka katikakti ya gari akisema shusha konda hapo,konda akasema wapi?,baba akajibu hapo hapo,Mmmmmmmmm?,”Samahani konda nilikuwa nashuka bucha nimejisahau” alisikika yule baba akisema,Mmmmmmmmm?.Ndipo nilipoona kila mtu karudi katika hari yake ya kawaida na wengine wakashuka hapo kama watu sita hivi.Nikajiuliza je walikuwa wanawaza nini? Mpaka wapitishwe kituoni?.Je walikuwa katika taswila kama yangu?,au uchovu wa kazi?

    Kati ya wale walioshuka pale njiani(sio kituoni) baba mmoja akasema akimwambia yule mama mjamzito “POLE SANA MAMA NA MIMI NAKUHAIDI SITOMPA KURA KIKWETE”akatelemaka.Tunavuka stopover na ni saa 3:30 usiku,kila mtu kaanza kusema lake”KIKWETE HANA AKILI”alisikika baba mmoja,”KIKWETE NI MGONJWA” alisikika dada mmoja,”WANAIGEIZA NCHI YA FAMILIA KWANI HAPA TUNATAWALIWA KIFALME” alisikika kaka mmoja.Ni saa 3:45 nashuka kibanda cha mkaa na niliposimama nikwaambia abilia “HUYO NDIO RAIS WENU HATA KIWA CHIZI SI MLIMCHAGU WENYEWE” nikajibiwa na konda “SHUKA UKO NA NENDA ZAKO”,Mmmmmmmm ata konda?

    Nikiwa njiani nakwenda kwangu nikawa natafakari “JE YALE MACHOZI YA MAJI YALIYONDONDOKA NDANI YA DALADALA LEO”je ni ya bure tu?,na je “IPO SIKU YATALIPWA”?,na je “IPO SIKU YATAGEUKA KUWA NI MACHOZI YA DAM”? nisingependa ilo tafakari langu la mwisho litokee.

    Je wewe unatoa machozi gani au maneno agani?,je machozi ya furaha? Au ya uzuni kama yule mama mjamzito?au maneno ya kumtukana rais wako kama wale watu kwenye daladala.Kazi kwako. Nikipata nauli kabla ya UCHAGUZI nitakwenda kanyigo nimuulize babu “JE BABU UMESHAWAI KUONA KICHUGUU CHA SENENE”?.

SUBSCRIBE- Andika email yako hapa utumiwe habari mpya

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008 modified by Subi nukta77

Go Back to TOP