Serikali Tatu Zitapunguza Gharama za Uendeshaji
Serikali Tatu Zitapunguza Gharama za Uendeshaji
Gharama za ziada zinaweza kuepukwa mathalan kwa kuiondosha Ofisi ya Makamu wa Rais na kuivunjilia mbali ofisi ya Waziri Mkuu butu asiye na meno hata kucha
Kinachoelekea kuuteka mjadala wa
katiba mpya hivi sasa ni pendekezo la serikali tatu. Naunga mkono serikali tatu
kwa kuwa kiuhalisia imethibitika kuwa vigumu kuwa na serikali moja kwa
kisingizio cha kumezana. Na hizi mbili zimechusha kero zake na viraka vimekuwa
vingi mno kiasi kwamba nguo yetu hii Muungano itatatuka pasipo kujitafakari
upya.
Sababu kubwa inayoonekana kuwa
nzito ni kuhusu gharama. Ninachangia hili la gharama kwenye makala hii fupi.
Serikali tatu zinaweza kuokoa sana gharama
ikiwa tutaacha hofu ya kisichojulikana na kujikita katika kufikiri kwa kutumia
mbongo na sio visigino nk kama walivyofanya kina Nyerere na Karume
walivyofikiri kwa mbongo zao na nia na dhati ya mioyo kabisa. Nasi sasa tunao wajibu; Tukiutimiza wajibu huu
tutatuzwa na tukiutelekeza tutatwezwa maana ilishanenwa Likulli
ajalin kitab', yaani kila zama ina kitabu
chake,”
Gharama za ziada zinaweza
kuepukwa mathalan kwa kuiondosha Ofisi ya Makamu wa Rais na kuivunjilia mbali
ofisi ya Waziri Mkuu butu asiye na meno hata kucha (ofisi na sio mhe Pinda). Viongozi wakuu wa serikali hizi mbili
yaani Tanzania Bara na Zanzibar
ndiyo
watakuwa wasaidizi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na mawaziri
wachache wa kisekta watakuwa wasaidizi wa karibu wa viongozi wakuu wa serikali
hizi mbili za Tanzania bara na Zanzibar .
Bajeti inayotumika sasa kuendesha
ofisi ya Rais itatumika kuendesha ofisi ya Rais wa Muungano sambamba na
kusimamia masuala ya Muungano. Gharama za uendeshaji wa ofisi ya Waziri Mkuu na
sehemu ya bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Rais sasa zitatumika kuendesha Ofisi ya
Kiongozi wa Serikali ya Tanzania Bara (bila kujali cheo cha kiongozi huyo ataitwaje).
Bajeti za wizara ambazo si za muungano (hizo zipo hata sasa) hata hivyo
zinaweza kupunguzwa.
Gharama za uendeshaji wa serikali
ya Zanzibar wala haina haja hata kuhofia maana hizo zipo hata sasa.
Kwa upande wa Bunge
Bunge la Muungano halitakuwa na
haja ya kukaa muda mrefu kama ilivyo sasa kwani masuala ya muungano si mengi
kiasi hicho. Gharama za muda utakaookolewa zitatumika kuendesha bunge la Bara.
Hali kadhalika Bunge la Tanzania Bara litapungua ukubwa wake na hivyo kupunguza
gharama tofauti na hivi sasa ambapo wakati wa kujadili masuala ya bara yasiyo
ya muungano wabunge kutoka zanzibar huwa hawatoki wanakuwepo na posho wanalamba
kama kawaida ilhali mijadala inayoendelea inahusu mambo ‘yasiyowahusu’.
Gharama gani tunazihofia? Mambo
yasiyo ya Muungano kwa upande wa Visiwani yanajadiliwa na baraza la wawakili
hata sasa. Serikali tatu zinaweza kupunguza gharama hata zile za vikao vya
mapatano na kutanzua kero za muungano wa serikali mbili za sasa ambazo
hazitanzukiki.