Serikali Tatu Zitapunguza Gharama za Uendeshaji
Serikali Tatu Zitapunguza Gharama za Uendeshaji
Gharama za ziada zinaweza kuepukwa mathalan kwa kuiondosha Ofisi ya Makamu wa Rais na kuivunjilia mbali ofisi ya Waziri Mkuu butu asiye na meno hata kucha
Kinachoelekea kuuteka mjadala wa
katiba mpya hivi sasa ni pendekezo la serikali tatu. Naunga mkono serikali tatu
kwa kuwa kiuhalisia imethibitika kuwa vigumu kuwa na serikali moja kwa
kisingizio cha kumezana. Na hizi mbili zimechusha kero zake na viraka vimekuwa
vingi mno kiasi kwamba nguo yetu hii Muungano itatatuka pasipo kujitafakari
upya.
Sababu kubwa inayoonekana kuwa
nzito ni kuhusu gharama. Ninachangia hili la gharama kwenye makala hii fupi.
Serikali tatu zinaweza kuokoa sana gharama
ikiwa tutaacha hofu ya kisichojulikana na kujikita katika kufikiri kwa kutumia
mbongo na sio visigino nk kama walivyofanya kina Nyerere na Karume
walivyofikiri kwa mbongo zao na nia na dhati ya mioyo kabisa. Nasi sasa tunao wajibu; Tukiutimiza wajibu huu
tutatuzwa na tukiutelekeza tutatwezwa maana ilishanenwa Likulli
ajalin kitab', yaani kila zama ina kitabu
chake,”
Gharama za ziada zinaweza
kuepukwa mathalan kwa kuiondosha Ofisi ya Makamu wa Rais na kuivunjilia mbali
ofisi ya Waziri Mkuu butu asiye na meno hata kucha (ofisi na sio mhe Pinda). Viongozi wakuu wa serikali hizi mbili
yaani Tanzania Bara na Zanzibar
ndiyo
watakuwa wasaidizi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na mawaziri
wachache wa kisekta watakuwa wasaidizi wa karibu wa viongozi wakuu wa serikali
hizi mbili za Tanzania bara na Zanzibar .
Bajeti inayotumika sasa kuendesha
ofisi ya Rais itatumika kuendesha ofisi ya Rais wa Muungano sambamba na
kusimamia masuala ya Muungano. Gharama za uendeshaji wa ofisi ya Waziri Mkuu na
sehemu ya bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Rais sasa zitatumika kuendesha Ofisi ya
Kiongozi wa Serikali ya Tanzania Bara (bila kujali cheo cha kiongozi huyo ataitwaje).
Bajeti za wizara ambazo si za muungano (hizo zipo hata sasa) hata hivyo
zinaweza kupunguzwa.
Gharama za uendeshaji wa serikali
ya Zanzibar wala haina haja hata kuhofia maana hizo zipo hata sasa.
Kwa upande wa Bunge
Bunge la Muungano halitakuwa na
haja ya kukaa muda mrefu kama ilivyo sasa kwani masuala ya muungano si mengi
kiasi hicho. Gharama za muda utakaookolewa zitatumika kuendesha bunge la Bara.
Hali kadhalika Bunge la Tanzania Bara litapungua ukubwa wake na hivyo kupunguza
gharama tofauti na hivi sasa ambapo wakati wa kujadili masuala ya bara yasiyo
ya muungano wabunge kutoka zanzibar huwa hawatoki wanakuwepo na posho wanalamba
kama kawaida ilhali mijadala inayoendelea inahusu mambo ‘yasiyowahusu’.
Gharama gani tunazihofia? Mambo
yasiyo ya Muungano kwa upande wa Visiwani yanajadiliwa na baraza la wawakili
hata sasa. Serikali tatu zinaweza kupunguza gharama hata zile za vikao vya
mapatano na kutanzua kero za muungano wa serikali mbili za sasa ambazo
hazitanzukiki.
1 comments:
Tume ya Mabadiliko ya Katiba Mpya, imewabeza watu, hususan wanasiasa wanaosimama majukwaani kueleza Muundo wa Muungano wa Serikali tatu utaongeza gharama za kiuendeshaji kuwa ni uongo na sababu hizo hazina tija.
Mjumbe wa Tume hiyo, Humphrey Polepole alisema hayo jana wakati wa mkutano wa kuijadili Rasimu ya Mabadiliko ya Katiba Mpya mbele wa Wajumbe wa Baraza la Wilaya ya Nanyumbu Mkoani Mtwara.
Alisema Muundo wa Serikali tatu hauna gharama zozote kwani chanzo cha mapato cha kuongoza Serikali ya Muungano kuwa tayari kimebainishwa.
Polepole alisema gharama za kuongoza Serikali hiyo zitatokana na Kodi ya Ushuru wa Bidhaa ambapo jumla yake zinazokusanywa si chini ya Sh1 trilioni.
“Mpaka sasa Serikali ya Muungano inakusanya zaidi ya Sh3 trilioni hivyo kama itatumika Sh1 trilioni na zitakazobaki zitaelekezwa katika shuguli zingine, fedha zitakuwepo,” alisema Polepole na kuongeza:
“Nashangaa wanasiasa wanaosimama majukwaani kueleza wananchi kuwa kutakuwa na mzigo wa gharama, hii si kweli kwani Tume tumekwisha bainisha chanzo chake cha mapato na hao wanaozungumza hayo hawafuatilii mchakato kwa umakini.”
Alisema uchambuzi walioufanya juu ya kodi inayokusanywa mwaka 2003/04 zilikusanywa jumla ya Sh500 bilioni na mwaka 2011/12 zilikusanywa Sh1 trilioni ambapo kila mwaka mapato hayo yanaongezeka.
“Uzoefu unaonyesha kila mwaka mapato yanaongezeka hivyo uwepo wa Muungano wa Serikali tatu ni dhahiri hautaathiri kitu chochote na utasaidia kutatua kero zilizopo zinazojitokeza kila mwaka kila kukicha,” alisema Polepole
Polepole aliwataka Wananchi kutokuwa na shaka na mapendekezo hayo ya Tume juu ya Muundo wa Muungano kuwa wa Serikali tatu kwani utapunguza malalamiko ya muda mrefu yaliyopo.
“Hivi sasa kuna kero zaidi ya 47 na kwa Muungano huu uliopo hautamaliza na wala hauwezi kuyafanyia kazi lakini kutokana na mapendekezo ya Tume ya Serikali tatu ninahakika yatapungua na kila upande kutokuwa na malalamiko,” alisema Polepole.
Polepole amesisitiza kwa kuwaomba wananchi kuendelea kutoa maoni katika hali ya kutoshinikizwa kwa namna yoyote.
“Kila mtu anapaswa kuwa huru kutoa maoni yake bila kuogopa chochote. Lengo la uwepo wa katiba mpya ni kujua hitaji hasa la wananchi ni nini na kwamba katika kutoa maoni wananchi wanapaswa kufanya hivyo bila woga,” alisisitiza Polepole.
soma zaidi hapa:
http://www.mwananchi.co.tz/habari/habari-ya-ndani/Tume--Hakuna--gharama-kuendesha-Serikali-tatu/-/1724700/1932458/-/nuvbe6z/-/index.html
Post a Comment