Pekua/search

Saturday, May 31, 2008

Mulinda; Msanii wa Injili aliyepania kuimba ‘Live’

KARIBU kila fani hapa nchini, kwa njia moja au nyingine imewahi kulalamikiwa kuvamiwa na wababaishaji ambao hufanya kazi au kutoa huduma zisizokidhi haja kwa walengwa, wala ubora wa bidhaa husika.

Uimbaji wa nyimbo za Injili ni miongoni mwa fani ambazo licha ya kwamba ni burudani, ni ajira ambayo huifanya fani hiyo ithaminiwe na hivyo mazingira hayo kuvutia baadhi ya watu wasio waaminifu.

Katika siku za hivi karibuni, kumekuwapo na ongezeko kubwa la waimbaji binafsi wa nyimbo za Injili ambao kwa majira na maeneo tofauti wamekuwa wakizindua albamu zao kwa kuufahamisha umma kuhusu kazi zao.

Pamoja na mambo mengine, wageni wa heshima katika matamasha hayo ya uzinduzi wa albamu hizo, wamekuwa wakitoa changamoto mbalimbali pindi wanapotakiwa kutoa nasaha zao katika hafla hizo.

Akinukuliwa na vyombo mbali mbali vya habari mapema mwezi uliopita katika tamasha la uzinduzi wa albamu ya Mwimbaji Vita Kissi Tabata Segerea Dar es Salaam, mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya African Evangelical Enterprises (AEE) aliwataka wasanii wa nyimbo za Injili nchini kuwa waadilifu ili kuepusha uwezekano wa kuwepo vitendo vya kifisadi katika fani hiyo.

Aidha, akitofautisha uimbaji wa nyimbo za Injili na zile za bongofleva, mkurugenzi huyo alisema, tofauti na nyimbo za ‘bongofleva’ jukwaa la nyimbo za Injili ni eneo ambalo huhitajika uadilifu kutokana na umuhimu wa huduma hiyo kwa jamii.

Pamoja na kwamba fani hiyo ni ajira, Masangakulangwa alikemea tabia ya baadhi ya wasanii wa nyimbo za Injili hapa nchini kufanya huduma zao kibiashara zaidi kuliko kihuduma.

Fredrick Mulinda mkazi wa Mbezi Dar es Salaam ni msanii chipukizi wa nyimbo za Injili nchini ambaye amerekodi albamu yake ya kwanza yenye nyimbo kumi hivi karibuni.

Mapema akizungumza na safu hii, mwishoni mwa wiki Dar es Salaam anasema, albamu hiyo inakwenda kwa jina la Moyo wangu, na kwamba alirekodia studio ya Don Bosco ya Upanga Dar es Salaam. Anasema, albamu hiyo ipo katika mfumo wa CD na Audio (kaseti) ambayo wakati wowote itaingia sokoni katika kukosha nyoyo za wapenzi wa nyimbo zenye mahadhi ya Injili ‘gospel flavor’.

Msanii huyo ambaye anatokea katika familia ya kidini anasema, yeye na washauri wake wapo katika dakika za mwisho mwisho kwani anatarajia kuingia sokoni katika jukwaa zima la nyimbo za Injili ndani na nje ya nchi kwa ‘staili’ ya tofauti.

Mulinda, ambaye kitaaluma ni mwanasayansi wa Afya ya Mazingira aliyehitimu katika Chuo Kikuu Kishiriki cha Muhimbili (MUCHS) anasema, mashabiki na wapenzi wa nyimbo za Injili wakae mkao wa kula kwani dhamira yake ni kufikisha ujumbe unaobadilisha tabia na hali duni za watu na hajaweka kipaumbele cha kutafuta pesa.

Anasema, lengo la msingi la kuimba katika maisha yake kwanza ni kujitokeza hadharani ili kipaji chake alichokifanyia majaribio kwa miaka mingi kiweze kuonekana na pili matokeo ya kipaji hicho iwe ni fursa ya kipekee kuifikishia jamii ujumbe wenye maudhui mbali mbali sambamba na kumtumikia Mungu.

Kihistoria msanii huyu anaonekana tofauti kidogo na wenzake katika fani hiyo kwa sababu kipaji chake kililelewa vema na baba yake mzazi Fulgence Mulinda (sasa marehemu) aliyekuwa Askofu wa Kanisa la Pentecostal Holliness Mission (PHM) Jimbo la Kagera kwa zaidi ya miaka 15 iliyopita.

Kama hilo halitoshi, Fanuel Mulinda ambaye ni kaka yake wa kuzaliwa, ni Mchungaji ambaye na yeye amejaliwa kuwa na kipaji cha kuimba cha aina yake na hivyo ‘kumpiga msasa’ mara kwa mara ili ang'ae katika medani ya nyimbo za Injili.

Mulinda anasema anawashukuru wahisani mbalimbali waliofanikisha kurekodi albamu yake hiyo kwani msanii kufikia hatua ya kurekodi katika hali ya kawaida huwa ni jambo la kutia moyo na linaloonyesha wazi kuwa msanii husika yupo makini katika kazi yake.

“Kusema kweli tangu mchakato wa kutoa albamu hii uanze miezi kadhaa iliyopita nilikutana na misukosuko ya hapa na pale ambayo huwa haikwepeki kutokana na hasa ufinyu wa bajeti ya kufanyia shughuli hiyo, lakini hii ni changamoto kwangu ili nijipange zaidi kwa albamu nyingine zijazo Mungu akitujalia,” anasema.

Anasema, anachokifanya hivi sasa, ni kuendelea kumuomba Mungu malengo yake yatimie kama alivyopanga, hatimaye azalishe nakala nyingi kadiri iwezekanavyo na kuzisambaza kwa wateja. Katika albamu hiyo amewashirikisha waimbaji watatu ambao ni Nicodemus Shaboka wa CAG Urafiki, Angel Bernard (Amana Vijana Center) na Hossiana Masang'ula (PHM Salasala) wote wa Dar es Salaam.

Mulinda hakuibuka hivi hivi, hadi kufika hapo alipo sasa, kapitia maeneo mbali mbali ambayo yalikuwa ni shule tosha kwake hadi kufaulu kuwa mwimbaji chipukizi wa ‘gospofleva’ anasema, mwaka 1995 hadi 1998 akiwa Ihungo Sekondari Bukoba Mjini akiwa na kikundi cha Voice Boys Fellowship (VBF) ndipo nyota yake ilipoanza kun’gara kiuimbaji.

Anasema, kundi la Voice Boys Fellowship lililokuwa na vijana 25 yeye alikuwa tegemeo kwao kwani kwa kiasi fulani aliwasaidia katika kuwafundisha kuimba kwa ustadi unaotakiwa. Anasema, upako wa uimbaji ulimsukuma hadi alipomaliza shule hapo Ihungo sekondari hadi alipojiunga na Mkwawa High School ya Iringa mwaka 1999 hadi 2001.

Iringa Pentecostal Youth Association (IPYA) ni kikundi kingine ambacho baada tu ya yeye kujiunga kama mwanachama muda mfupi tena kipaji chake kilionekana kun’gara, jambo lililosababisha apewe wadhifa wa kuwa mwalimu wa kwaya shuleni hapo wakati huo ikijulikana kama Agape kwaya. Agape kwaya wakati huo ikiwa na waimbaji watano, ilikuwa chini ya uongozi wake, walitunga nyimbo saba ambazo kati ya hizo, wimbo wa “Mwokozi Yesu ninakupa sifa ulikuwa unaongoza”.

“Kikundi kile kwa kweli kilikuwa ni wamisionari ambao tulikuwa tukipeleka huduma ya uimbaji na neno la Mungu katika makanisa na jamii ya watu mbali mbali popote tulipoalikwa mkoani Iringa,” anasema. Mulinda anamtaja Cyprian Gabriel kama swaiba wake wa karibu ambaye alikuwa naye bega kwa bega katika kuhakikisha kuwa, Agape kwaya inakosha nyoyo za wasikilizaji, hasa watu wa Mungu mkoani Iringa kwenye mikutano na makongamano mbali mbali.

Anasema, alipomaliza masomo Mkwawa High School, ulikuwa ndio mwanzo wa kuingia katika zama mpya kiuimbaji kwani mwaka 2002 hadi 2005 akiwa Chuo Kikuu Kishiriki Muhimbili (MUCHS) alikutana na hamasa tofauti tofauti kutoka kwa vijana wenzake wenye kipaji cha kuimba kama yeye, jambo lililompa msukumo zaidi katika kutaka kutimiza ndoto zake katika fani hiyo.

Akiwa MUCHS kati ya mwaka 2005 na 2006 ndipo mazingira yalipomruhusu kutimiza ndoto zake kwa njia yoyote, jambo lililomfanya aanze kuwa na muda wa kutosha kutulia mbele za Mungu kwa ajili ya maelekezo maalum baada ya kumaliza masomo yake.

Anasema, mapema mwanzoni mwa mwaka huu alianza rasmi kukusanya nyimbo zake na hatimaye akafanikiwa kurekodi albamu yake hiyo. Matarajio yake ni kuwa na kikundi kitakacholeta mapinduzi katika fani ya uimbaji kwa kuondoa mfumo wa kuimba kwa kutumia CD na badala yake kuimba ‘live’.

Mulinda amefunga pingu za maisha na Lucy Kyombo mapema mwaka jana, wamejaliwa kupata mtoto mmoja anayeitwa Michael mwenye miezi miwili sasa.

Msanii huyo ni mtaalamu wa mazingira katika Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) wakati mkewe ni muuguzi Hospitali ya Taifa ya Muhimbili wanaishi Mbezi Dar es Salaam.

CHANZO:
Innocent MallyaDaily News; Friday,May 30, 2008 @20:05

0 comments:

SUBSCRIBE- Andika email yako hapa utumiwe habari mpya

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008 modified by Subi nukta77

Go Back to TOP