Pekua/search

Friday, July 3, 2009

TUJADILI MFUKO WA KUCHOCHEA MAENDELEO YA JIMBO (CDCF)

Wakati nchini Kenya Kunafukuta kuhusu CONSTITUENCY DEVELOPMENT FUND (CDF), Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania liko mbioni kupitisha muuswada wa kuanzisha kitu kama hicho hicho (Constituency Development Catalyst Fund) kwa madai kwamba kitakuwa bora zaidi na chenye manufaa nchini katika kuchochea maendeleo. Wamedhamiria na kujipanga vilivyo. Soma tamko la Policy Forum hapa.

Jumapili iliyopita nilikuwa miongoni mwa 'wawakilishi' wa AZAKI (CSOs) waliohudhuria kikao/mkutano wa kukuwadisha ushirikiano baina ya wabunge na AZAKI uliofanyika ukumbi wa Msekwa mjini Dodoma.

Jambo lililojitokeza wazi wazi ni wabunge kutumia kila namna ikiwemo kushambulia AZAKI, kutaka ziunge mkono MFUKO WA MAENDELEO YA JIMBO - CDCF. Hapa sitazungumza kuhusu ni kwanini AZAKI 'zinapinga' mfuko huo ama ni kwanini wabunge wanaushupalia sana.

Mchango wangu unajikita katika hoja moja iliyojengwa na wabunge na ambayo kwa kiasi wana AZAKI, kwa maoni yangu walionekana kuikubali. Nayo ni matarajio ya wananchi kupewa fedha na wabunge kwa ajili ya matatizo yao na yale yanayohusu maendeleo yao. Mheshimiwa Simbachawene, yeye alieleza kwa lugha fasaha na rahisi kabisa, kuwa wabunge wanekuwa ATM! Hapo ndipo nguvu ilipo kwao kutaka CDF ipitishwe ili wasaidie kuchochea 'maendeleo' ya watu wao.

Ninalojiuliza hapo, na ambalo iwapo mkutano ule ungekuwa na fursa ya kujadiliana ningewauliza waheshimiwa hawa, ni Je miongoni mwa wajibu, majukumu na kazi za wabunge hilo la kuwa ATM limo?

Nadhani, hapo ni suala la kimtizamo. Kutokana na kutojiamini, wabunge wamependa njia za mkato za kutafuta kukubalika, moja na maarufu ni kugawa vijisenti kwa wapiga kura. Wananchi waliowengi wamekengeuka mwisho wa siku, wamejenga matarajio ya kupata fedha kutoka kwa mbunge. hoja hii haina mashiko.

Ningepata fursa ya kuchangia siku ile, nilijiandaa kushauri badala ya wabunge kukomalia CDCF (ambayo itadhoofisha uwezo na madaraka yao ya "kuisimamia na kuishauri Serikali", kwa niaba ya wananchi), ningeshauri AZAKI zisaidie kuelimisha jamii kuachana na dhana na mtazamo wa kuwaona wabunge kuwa ATMs.

Ningepata fursa (kumbuka nilihudhuria, na kuhudhuria si lazima kuhusishe ushiriki) ningehoji zitakakotoka fedha hizo (tena katika kipindi hiki cha mdororo wa uchumi duniani na ni kwanini fedha hizo kama zimekosa kazi nyingine ya kufanya zinashindikana kuingizwa kwenye mifumo iliyopo, mathalani serikali za mitaa.

Huu ndiyo mchango wangu
Nawasilisha.

0 comments:

SUBSCRIBE- Andika email yako hapa utumiwe habari mpya

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008 modified by Subi nukta77

Go Back to TOP