Pekua/search

Tuesday, September 22, 2009

KUJIFUNZA KWA SALMA KIKWETE KUHUSU KISWAHILI


Matumizi ya Kiswahili: Tuna la kujifunza kwa Mama Salma Kikwete.
Na Lingson Adam

Wadau makala haya yalichapishwa kwenye gazeti la Sauti Huru mwezi Mei mwaka huu (2009) kuendeleza mjadala wa MATUMIZI na Fahari yetu kwa Kiswahili nimeona vema kuuweka hapa kama sehemu ya kuendeleza mjadala.

Pichani Mama Salma akikabidhi kabrasha kuhusu mipango ya WAMA kwa naibu mkurugenzi mtendaji wa UNICEF mama Hilde Johnson ambaye anakichapa Kiswahili barabara.Picha kutoka blogu ya Michuzi

Tangu alipoingia madarakani, Rais wa awamu ya nne Jakaya Kikwete, mkewe, first Lady Salma Kikwete pichani (kutoka blogu ya Michuzi)
kushoto, amekuwa mstari wa mbele katika harakati mbalimbali. Harakati zake hizo zimejipambanua zaidi katika kuanzisha na kuendesha
kwa ufanisi shirika la Wanawake na Maendeleo – WAMA, ambalo yeye ni mwenyekiti.

Katika harakati hizo mama Salma, amekuwa akikaribisha na kupokea wingi wa wageni mbali mbali kutoka mataifa ya karibu na mbali.

Mara nyingi, kama si zote, mama Salma amekuwa(alikuwa) akitumia Kiswahili katika hotuba zake kwa wageni wake. Ni katika suala hili ambapo nadhani mama Salma anastahili pongezi, kuungwa mkono na kujifunza kutoka kwake.

si ajabu kwamba mwanzoni wengi wetu tulidhani ni kutokana na yeye kutokuwa bingwa katika lugha ya Kiingereza, lakini nadhani mpaka sasa tumejihakikishia kwamba tulichemka. Mama huyu Mwalimu kitaaluma na kitaalamu, anakijua Kiingereza vizuri kabisa, walau sawa tu na viongozi wetu wa kiume na wakike waliowengi.

Mrengo aliouchukua mama Salma nadhani ni wa maksudi kabisa. Aliamua toka mwanzo kabisa kujipambanua kuwa ni Mtanzania anayejivunia Kiswahili.

Mama Salma amekuwa mstari wa mbele kueleza bayana umuhimu wa Kiswahili. Akiwa safarini nchini Marekani na Uingereza hivi karibuni, alitoa changamoto kwa watanzania waishio katika nchi hizo kuongea Kiswahili fasaha na kujivunia lugha hiyo adhimu. Mama Salma alieleza bayana kwamba Kiswahili ni raslimali muhimu ya watanzania

Mama Salma amekuwa mara kwa mara akiwashaajisha watanzania kuwa ni muhimu waenzi utamaduni wao, na kwa kutumia Kiswahili watakuwa wametekeleza suala hilo kwa namna ambayo ni ya msingi sana pengine kuliko njia nyinginezo za kujipambanua kiutamaduni.

Katika suala hili mama Salma amejitoa na ametutoa kimasomaso na kwa hakika amekuwa mfano hata kwa mumewe, Rais wetu Jakaya Kikwete ambaye naweza kusema anakionea aibu Kiswahili.

Rais kupoteza fursa

Rais Kikwete mara nyingi amekwama kutumia fursa nyeti za kuitambulisha Tanzania kuwa mama au baba wa Kiswahili. Mathalani alipigwa mwereka na Rais wa Kenya Mwai Kibaki na Waziri Mkuu wake Raira Odinga huko Nairobi, mwanzoni mwa mwaka jana katika hadhara muhimu kabisa ya kimataifa. Baada ya kufanikiwa kuwaweka pamoja ndugu hao wa Kenya, Rais Kikwete kwa nafasi yake akiwa kiongozi mkuu wa Umoja wa Afrika wakati huo, alitoa hotuba yake kwa Kiingereza.

Kama Rais wa Tanzania anatoa hotuba kwa Kiingereza katika eneo la Afrika Mashariki, nani abebe bendera ya Kiswahili duniani? Tofauti na kiongozi huyo wa Umoja wa Afrika, 'faraja' ikaja pale Odinga na Kibaki walipohutubia kwa Kiswahili. na ndiyo maana ninasema walimpiga mwereka Kikwete wetu hawa Wakenya! na walitupiga mwereka mbaya sana watanzania wote hawa ndugu zetu!

Ni rahisi kuuchukulia kirahisi mfano huu, lakini uzito wa jambo linalofanywa na kiongozi wa jamii au nchi fulani hauwezi kupuuzwa. Afanyacho kiongozi wa watu, asemacho kiongozi wa watu kinabeba, kwa asilimia kubwa, nadhani kubwa kabisa, taswira ya jamii au taifa analoliongoza.

kwa hili, mtoto wa taifa la mbali aliyekuwa akisikiliza hotuba hizo na angetokea kuuliza wazazi wake ni lugha gani Kibaki na Odinga walikuwa wakiiongea na akaambiwa ni Kiswahili, basi atajua Kiswahili ni lugha ya Kenya. Haina ubaya wakenya kuongea Kiswahili, lakini utambulisho wetu unapotea. rais wetu alipoteza furasa. na amepoteza nyingi za aina hiyo. viongozi wetu wengi mawaziri kwa wanadiplomasia wengi wengine, wamepoteza fursa hizo

Kiswahili kama fursa na raslimali inayopotezwa

Tunayorekodi watanzaia, rekodi mbaya na chungu kuikubali. Tunaelezwa na wenzetu wa karibu na waliotoka mbali, naam hata sisi wenyewe tunajua na kufahamu kwamba tumebobea katika kupoteza ama kutotumia ipasavyo fursa nyeti za kutuendeleza. Moja ikiwa ni mlima Kilimanjaro, mlima mrefu kuliko yote barani Afrika.

Imeelezwa kwa miaka mingi kuwa pamoja na mwenyezi Mungu kutujaalia utajiri wa raslimali za kipekee Afrika na duniani, watanzania hatujaweza kuzitumia vema fursa na raslimali hizo kutusaidia kuishi vema zaidi. Mlima Kilimanjaro umekuwa kwenye rekodi ya juu kuwa umetumika kwa tija zaidi na jirani zetu wa Kenya kuvutia utalii. Ahueni imekuja walau miaka ya karibuni tulipoanza kuutangaza japo ‘kizembe zembe fulani’.

Kama kuongeza na chumvi kwenye jeraha la mtu, tumeelezwa na kuchekwa kuwa hatujatukuka duniani kuwa wauzaji wanaoongoza wa madini ya TANZANITE yanayopatrikana Tanzania pekee!

Kiswahili kama lugha ambayo licha ya historia yake kuhusisha upwa wa Afrika mashariki katika mapana na marefu yake, bado ni Tanzania ambayo ilijipambanua kihistoria kuwa mwenye kuitumia lugha hiyo kitaifa tangu wakati wa harakati za kupigania uhuru na baada ya uhuru.

Hata hivyo, hatujaitumia fursa ya kuwa ‘wamiliki’ wa lugha hii kututajirisha wakati ndiyo lugha pekee yenye uwezekano wa kuwa lugha ya mawasiliano kwa nchi zote za Afrika ya mashari kati na kusini. Hakuna lugha nyingine yenye fursa kama ya Kiswahili kwenye eneo hili. Lugha hii ingeweza kupanua soko letu la kuajirika ndani na nje ya mipaka yetu. Utashangaa leo hii, watanzania tukinyong’onyezwa nasi kunyon’gonyea kwa madai ya kizandiki eti ‘watanzania hatuajiriki sana kimataifa zaidi ya wakenya kwa vile hatujui Kiingereza!!’

Tungetumia vema raslimali hii ‘Kiswahili’ tungezalisha wakalimani na wafasiri makumi kwa maelfu duniani, tungezalisha walimu wa lugha hii adhimu maelfu kwa malaki duniani, na hizo ni fursa ambazo tunazihitaji. Taarifa zinaonyesha walimu wengi wa Kiswahili duniani wanatoka nchini Kenya!

Hatari ya watanzania kutokutumia kwa faida Kiswahili inaelezwa na kufupishwa vizuri zaidi kwa hadithi ya UBINGWA MA NANYIGU na NYUKI KATIKA KUTENGENEZA ASALI aliyoniambia mwalimu wangu mzee Millinga.

Kwa mujibu wa hadithi ya mwalimu wangu huyo manyigu ndiyo yalikuwa mabingwa duniani katika kutengeza asali. Maprofesa wa kufundisha wadudu wengine kutengeneza asali walikuwa ni manyingu na wala hapakuwepo viumbe wa kufafanana nayo. Chuo kikuu cha kutengeneza asali kilikuwa na wahadhiri, manyigu, wahadhiri wabobezi na wazamivu wapatao 20. Hawa walitegemewa dunia nzima.

Sifa hizo zilizovuma na kuenea kama moto wa nyika zilifanya wanafunzi manyigu kujisikia wa daraja la juu ‘na kweli walikuwa’ kwa hiyo hawakufanya sana bidii kujifunza. Lakini nyuki, ambao hawakuwa na historia ya ubingwa huo, waliona fursa hiyo, wakawa nafanya bidii sana katika kujifunza, wakaujua ujuzi kwa jasho lao na kukosa usingizi!

Siku ya siku wahadhiri manyigu walikwenda kwenye tafrija, walisafiri mbali upande wa bahari wa nchi hiyo kwa ndege. Baada ya kufurahi na jioni walipokuwa wakirejea majumbani kwao, lisilotarajiwa likatokea, ndege ikapata hitilafu, ikaanguka na mabingwa wote wakateketea!!!

Hapakuwa na mabingwa manyigu tena, wanafunzi wa asili ya manyigu, hawakuwa makini kupakuwa ujuzi kutoka kwa ndugu zao, bali walishiriki sifa tu ya jamii yao. Huo ukawa mwanzo wa wanafunzi na wanagenzi wa nyuki kuchukua usukani maana walifanya bidii sana katika masomo yao waliyafahamu maarifa na kuujua ujuzi, na ndiyo hadi leo nyigu hayatengezezi masega ikajaa zaidi ya kiganja, lakini nyuki, nani asiyemjua?

Waasisi wa taifa waliiona fursa katika Kiswahili kijamii, kisiasa, kiutamaduni na kiuchumi, ulinzi na usalama. Wakajifunga kukikuza na kukiendeleza Kiswahili, wakatujengea sifa ya Kiswahili, tukaheshimika duniani. Lakini leo sisi Tanzania kama taifa tunafanya juhudi zipi za kuhakikisha tunazalisha wahitimu wengi wa Kiswahili? Vyuo vikuu vyetu vinatoa mabingwa wangapi wa Kiswahili jamani? Hawawezi kuwa wengi, maana hata watoto wetu hawawezi kurithi fahari ya lugha ya Kiswahili, kwa vile wanatuona tunavyoona fahari kwenye shule za michepuo ya Kiingereza, almaarufu ‘English medium’, wana wetu wanatuona tunavyofarijika wakiongea kizungu cha ‘yesi dadi’, yesi mami’ sijui fotokopi tugeza na kazalika’. Wanachorithi ni kuwa fursa iko katika kiingereza, lakini kweli? Kiswahili hakina fursa? Kiswahili kwa Tanzania kama taifa kinayo fursa kubwa sana, lakini ni ile iliyopotezwa, ni fursa iliyopuuzwa.


Mwelekeo wa mama Salma hauna budi kuigwa na kuungwa mkono na Viongozi wetu wa Kitanzania. Tunafahamu wanajua Kiingereza vizuri. Lakini wanalo jukumu la msingi kabisa la kukienzi Kiswahili. Wanalojukumu la Kukieneza na kukitangaza Kiswahili. Wanawajibika kukikona Kiswahili kama raslimali adhimu pengine hata zaidi ya Tanzanite, ambayo ikichimbwa inatoweka moja kwa moja.

Viongozi wetu katika ngazi zote, zaidi yetu sisi sote, wanalo jukumu la kukitumia Kiswahili kama fursa muhimu ya ajira. Viongozi wetu wanapaswa kutumia Kiswahili na hivyo kututafutia vijana wa kitanzania kazi za ukalimani, ufasiri na ualimu wa lugha hiyo huko ughaibuni. Wakiongea Kiswahili bila aibu haya yatawezekana sana.

Ni mara nyingi viongozi wetu wametumia Kiingereza pasipo hata na ulazima wa kufanya hivyo. Akiwepo mgeni mmoja tu kutoka nchi za mbali, basi viongozi wetu watamwaga Kiingereza, hata kama anakijua kidogo Kiswahili mgeni huyo.

Inafahamika wazi mathalan, kwamba Rais wetu akienda na ujumbe wake Uingereza, hawezi kuwafanya viongozi wa nchi hiyo wazungumze Kiswahili kkwa ajili yake. Vivyo hivyo akienda Uchina na Japani, watazungumza lugha zao viongozi wa nchini hizo, na ujumbe wa Tanzania utawasiliana na wenyeji wao kupitia Wakalimani na Wafasiri. Hiki ndicho alichokianzisha mama Salma. Anakimwaga Kiswahili mtoto wa Kitanzania.Wageni wake wanapata fursa ya kuuonja utamu wa lugha hii adhimu.

HONGERA MAMA SALMA. ENDELEA. KANYAGA TWENDE, HAKUNA KURUDI NYUMA. MJENGA NCHI NI MWANANCHI MWENYEWE.Inawezekana kabisa, isingekuwa utashi wa viongozi waasisi wa taifa hili, hata majeshi yetu yangekuwa yanatumia kiingereza katika kuamrisha gwaride.

Inaaelezwa kwamba waasisi hao wakasema hapana, na taarifa zinaeleza kuwa waliobuni na kufasiri amri zinazotumika jeshini wala hawakuwa na kiwango kikubwa cha elimu kama tulivyo wengi wetu 'waswanglishi' wa hivi sasa. Haidhuru hata kama walianza kwa kusema, 'nyumaaaaaazi geuka! kuliaaaaaaaaz geuka, mbeleeeeeeeee tembea!'shotu kulia, shotu kulia, shotu kulia!!! Mwisho wa siku Kiswahili kimetamalaki jeshini kwa kiwango kizuri kabisa.

Wakati umefika kwa viongozi wengine kukienzi Kiswahili kwa kukitumia, hususan katika hotuba zao ndani ya nchi. Bungeni ndiyo kabisaaaa.

Changamoto kwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa

Balozi zetu nje ya nchi zianzishe vituo vya kufundishia Kiswahili kama vile zifanyavyo balozi za Ufaransa na Uingereza na nchi nyingine. Balozi zetu zifanye au zizidishe juhudi za maksudi kukitangaza Kiswahili, hata kama hakutakuwa na anayesikiliza, lakini na tufanye hivyo.

Balozi zetu zifanye kasi kubwa zaidi kuzishawishi taasisi za elimu kwenye nchi wanakotuwakilisha ili zianze kufundisha lugha ya Kiswahili, na wakati huo huo ziwe na orodha na mawasiliano ya vijana waliohitimu katika lugha hii ili wakihitajika tu, basi waweze kuwapata kirahisi. Tanzania tuendelee kuwa ‘wamiliki’ wa Kiswahili!!!

Mungu kibariki Kiswahili. Mungu tubariki Watanzania.

3 comments:

Asifiwe October 3, 2009 at 6:25 AM  

Mmmmh kweli ulichosema kinatikisa sana mpaka nywele zinasisimka, kwa kweli pasipo maono tutaangamia.Tunakosa utambulisho na mwisho wa siku tutakuwa hatujui chochote maana kuna msemo(tafsili kutoka kizungu)ANAYENG'ANG'ANIA YOTE SI MJUZI WA YOTE ..kama tafsili si nzuri waungwana mnisamehe.(JAGGER OF ALL TRADES IS A MASTER OF NONE) Nimekuwepo huko shuleni yaani watoto hao wa medium kiswahili hawajui hata hicho kiingereza waingereza watusamehe tu.
Nadhani viongozi wetu wabadilike sasa waone kutumia kiswahili bado wanakuwa watu wa juu tu,wasidhani kutumia kiingereza ni ufahari bali wajue ni aina nyingine ya ukoloni ujiendelezao katika mawazo
Na sisi tuongozwao tuone kuendelea kutoheshimu lugha yetu ni ufukara wa mawazo
ADUMU ALIYESEMA KISWAHILI NDIO LUGHA YETU

Unknown August 17, 2012 at 5:59 AM  

Watu bado tuna utumwa, tena utumwa mbaya sana kuliko ule mkongwa, utumwa wa fikra ni mbaya sana, Kutothamini lugha/ utamaduni wako nakuthamini utamaduni wa mwingine unadhani uko huru?! Hawa viongozi wa Tanzania....wanasema maishabora...kutengeneza ajira..alafu wanasahau kuwa kiswahili ndio kinawaeza kufanikisha haya. Rais Bongo si Mtanzania lakini ameona umuhimu wa kiswahili na anhitaji walimu sasa kutoka Tanzania! Eti serikali pia haijaona hii ni fursa adimu. Tuamke watanzania kiswahili kinasifika dunia nzima! Hawa viongozi hawajali kabisa hata wanaofanya jitihada za kukitangaza kiswahili kwa Mfano kunachama cha wanafunzi wa kiswahili vyuo vikuu afrika mashariki CHAWAKAMA, chama hiki huwa kinafanya makongamano mara kwa mara ndani ya chi husika na mara moja kwa kila mwaka kuzunguka nchi wanachama, mwaka huu tutakuwa Bujumbura lakini tunapopita katika ofisi za serikali huhusani wizara kuomba ufadhili, majibu wanayotupatia ni ya kusikitisha sana, wantukatisha tamaa hadi tunaona sisi tunaosoma kiswahili kama tumepotea. Ukweli ni kwamba hatupati ushirikiano kutoka serikalini. Hii ni aibu. "KISWAHILI HAZINA YA AFRIKA KWA MAENDELEO ENDELEVU"
Mimi ni mpenzi wa kiswahili na mwanataaluma wa kiswahili.
benbisan@gmail.com

Unknown August 17, 2012 at 6:00 AM  

Watu bado tuna utumwa, tena utumwa mbaya sana kuliko ule mkongwa, utumwa wa fikra ni mbaya sana, Kutothamini lugha/ utamaduni wako nakuthamini utamaduni wa mwingine unadhani uko huru?! Hawa viongozi wa Tanzania....wanasema maishabora...kutengeneza ajira..alafu wanasahau kuwa kiswahili ndio kinawaeza kufanikisha haya. Rais Bongo si Mtanzania lakini ameona umuhimu wa kiswahili na anhitaji walimu sasa kutoka Tanzania! Eti serikali pia haijaona hii ni fursa adimu. Tuamke watanzania kiswahili kinasifika dunia nzima! Hawa viongozi hawajali kabisa hata wanaofanya jitihada za kukitangaza kiswahili kwa Mfano kunachama cha wanafunzi wa kiswahili vyuo vikuu afrika mashariki CHAWAKAMA, chama hiki huwa kinafanya makongamano mara kwa mara ndani ya chi husika na mara moja kwa kila mwaka kuzunguka nchi wanachama, mwaka huu tutakuwa Bujumbura lakini tunapopita katika ofisi za serikali huhusani wizara kuomba ufadhili, majibu wanayotupatia ni ya kusikitisha sana, wantukatisha tamaa hadi tunaona sisi tunaosoma kiswahili kama tumepotea. Ukweli ni kwamba hatupati ushirikiano kutoka serikalini. Hii ni aibu. "KISWAHILI HAZINA YA AFRIKA KWA MAENDELEO ENDELEVU"
Mimi ni mpenzi wa kiswahili na mwanataaluma wa kiswahili.
benbisan@gmail.com

SUBSCRIBE- Andika email yako hapa utumiwe habari mpya

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008 modified by Subi nukta77

Go Back to TOP