Pekua/search

Monday, September 14, 2009

MCHANGO WANGU KWA SERA MPYA YA ELIMU NA MAFUNZO 2009

UTANGULIZI:
Kwa ujumla Sera mpya inashughulikia masuala muhimu na ya msingi kama vile kupunguza umri wa kuanza shule kutoka miaka saba hadi mitano; kuwekwa kwa utaratibu wa kuwatambua na kuwaendeleza watoto wenye vipaji maalum; kuanzisha polytechnics; kuongeza masuala ya TEHAMA na UJASIRIAMALI kwenye mtaala; pamoja na masuala mtambuka.

MAONI:

Kifungu Na 5.3 (elimu ya chekechea) Tamko Na. 4 na 5.4 (elimu ya awali) tamko la 3; na 5.5 (elimu ya msingi) tamko la 7 katika suala la ufanisi katika kutoa elimu bora ya msingi kwa wote na Tamko Na. 1 na 2 kwenye suala la kubaini na kuendeleza vipawa na vipaji vya watoto.

Matamko yote haya yanahusu kuwekwa kwa utaratibu wa kuwatambua watoto wenye vipaji katika vituo vya chekechea, madarasa ya elimu ya awali na shule za msingi kwa lengo la kuwaendeleza katika ngazi za juu. Hata hivyo nia hiyo haijaakisiwa kwenye kifungu 5.7 kichohusu Elimu ya Ualimu. Hapana budi kuwepo tamko la sera linalotilia mkazo kutolewa kwa mafunzo mahsusi kwa walimu (kazini na tarajali) katika ngazi zote kuhusu utambuzi na uhuishaji wa vipaji na vipawa vya wanafunzi. Hali kadhalika, tamko hilo lijumuishe umuhimu wa kuandaliwa kwa walimu ambao pia watakuwa washauri wa mieleko na kazi (Career counsellors). Ni dhahiri kuwa mafunzo ya hivi sasa yanayotolewa vyuoni hayakidhi haja hizi.

Pia hapana budi mfumo rasmi wa upimaji uwe na tamko juu ya kuwekwa kwa utaratibu utakao tilia mkazo na kusaidia uibuaji wa vipaji

Kifungu Na 6. 9 Utawala bora liongezwe tamko la sera lenye kuelekeza kuwa serikali itajuisha misingi ya utawala bora kwenye mtaala wa elimu katika ngazi mbali mbali ili kuwaandaa wananchi wenye fikra huru, wenye kujiamini, wazalendo na wawajibikaji na wenye kuhimiza uwajibikaji wa serikali na viongozi.

suala:Utoaji wa chakula kwa wanafunzi


Pamoja na sera ya elimu na mafunzo ya 1995 tamko la sera 3.2.7 kuainisha kuwa serikali itaboresha programu za lishe na afya katika shule za msingi na vyuo; upo ushahidi kwamba zoezi hili ambalo umuhimu wake umethibitika na kuthibitishwa kitaalamu kwa tafiti mbalimbali, halikuweza kufanikiwa sana. Tafiti mbali mbali zinaonyesha kuwa, mbali ya maeneo yenye programu za utoaji chakula zinazosaidiwa na Mpango wa Chakula Duniani (WFP) kama Dodoma, Singida na Manyara na Arusha, pia yale yanayosimamiwa na miradi ya kijamii kama baadhi za wilaya za mkoa wa Kilimanjaro n.k; maeneo mengine ya nchi hayakuweza kufanikiwa sana katika kutekeleza zoezi hili.
Watoto wengi hususan wanatoka familia maskini zaidi wameendelea kwenda shuleni bila chakula. Wengine wamekuwa wakitoroka na wengine kuacha shule kabisa. Badala ya kutamka kimkakati zaidi, sera mpya imelieleza suala hili kijuujuu tu kama suala la huduma muhimu shuleni na vyuoni (Ukurasa wa 68), ambapo tamko la sera linaelekeza jukumu la serikali kuwa ni kuhimiza wazazi, jamii, serikali za mitaa na wadau wengine kuhakikisha kuwa huduma ya chakula bora......

Pendekezo
Liongezwe tamko la sera kuwa serikali kwa kushirikiana na wadau itaanzisha mpango kabambe wa utoaji chakula bora kwa wanafunzi wa shule za msingi wawapo shuleni ili kuwavutia kubaki shuleni na kuhakikisha wananufaika ipasavyo na matendo ya kujifunza.

Suala: usawa wa kijinsia:

Tamko Na. 6 kuhusu kuwekwa utaratibu wa kuwawezesha wanafunzi wa kike wanaopata ujauzito kuendelea na masomo baada ya kujifungua; halina budi kukamilishwa na tamko jingine lenye kuelekeza kuwa serikali itaifanyia mapitio sheria ya elimu na kuelekeza namna ya kuwabana watu wanaowapa mimba watoto wa shule na kudhibiti mazingira yanayopelekea watoto wa shule kupata ujauzito.

suala:makundi yenye mahitaji maalum.
kuwepo na tamko kuwa serikali itaelekeza utaratibu wa kuandaa mazingira rafiki, ikiwemo ujenzi wa miundombinu rafiki kwa wanafunzi na walimu wenye ulemavu mbali mbali

Suala:ufundishaji wa lugha: ukurasa wa 77
Kufuatia maelezo kuwa Kiswahili ni lugha adhimu ambayo nyumbani kwake ni nchini Tanzania hapana budi kuitazama lugha hii kuwa na hadhi zaidi ya kiingereza. Lugha ya Kiswahili ni tunu ya kipekee kwa nchi zaidi ya au sawa na mlima Kilimanjaro. Kiswahili ni miongoni mwa raslimali ambazo Tanzania inaweza kuzipeleka duniani katika dunia ya kitandawazi kwani imezidi kukua duniani.

Licha ya kigugumizi cha kuamua kuwa na lugha moja ya kufundishia nchini (KISWAHILI) Kuwepo na tamko la sera lenye kuelekeza kuwa wizara yenye dhamana ya elimu kwa kushirikiana na wizara nyingine kama yenye dhamana ya utamaduni na ya mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa itatoa maelekezo ya kukipa Kiswahili kipaumbele kama raslimali ya kipekee, kuikuza na kuitangaza, ikiwa ni pamoja na kuongeza idadi ya wahitimu mahiri wa lugha hii na kuendesha kampeni kabambe ya kuiingiza kwenye ulimwengu wa TEHAMA.

Suala: mfumo wa michepuo

Ukurasa wa 28 Tamko Na. 1 kuhusu kupanuliwa na kuendelezwa kwa utaratibu wa michepuo ya kilimo, biashara, ufundi na sayansi kimu.
kwa kuzingatia kuingizwa masuala ya TEHAMA na UJASIRIAMALI sambambaa na masuala mtambuka kwenye mitaala/mihtasari, ni vema sera itamke wazi kuwa itaifanyia mapitio mitaala ya masomo ya mchepuo (kilimo, biashara nk) ili kuifupisha na kuifanya iwe ya kivitendo na kijasiriamali zaidi au ikazie maarifa na stadi zinazopatikana kwenye mafunzo ya ujasiriamali. Vinginevyo hakuna faida kuwajazia wanafunzi mambo mengi ambayo hawataweza kumudu kuyashika.

Karibu tuchangie.

4 comments:

Anonymous September 14, 2009 at 5:14 AM  

nakubaliana nawe kuhusu suala la kutoa chakula shuleni lakini suala la kuendelea na masomo kwa wanafunzi waliopata ujauzito nafikiri kuwapa nafasi ya kuendelea na masomo sio suluhisho.
Nafikiri ni vema serikali ikafanta utafiti ni sababu ganni zinasababisha wanafuzi wapate mimba,je ni wanafunzi wangapi watarudi shule baada ya kujifungua?
Wanafunzi wenzao watawaonaje wenzao/watawaitaje?
je familia zao zina uwezo wa kuvilea vichanga hivyo?
Nionavyo mimi kama serikali imeamua wanafunzi waliopata mimba waendelee na masomo ni vema ikawajengea mazingira wanafunzi hao na kuwasaidia kupata mahitaji yao na watoto wao kwani naamini wengi wao wanatoka familia duni ambazo haziwezi kutimiza mahitaji ya mama na mtoto.

Adam September 14, 2009 at 5:22 AM  

Naam, ni kweli tunahitaji kupiga hatua zaidi ya hapo. Kwa hiyo kimsingi tukubaliane hawa watoto wanapopata mimba, ikitokea - waendelee na mmasomo baada ya kujifungua. Matatizo uliyo yataja ziwe ni changamoto za kuzikabili badala ya kuwa sababu za kufanya waendelee kubeba mzigo, ambao kimsingi umesababishwa na mfumo maisha ya jamii.kuwaacha nyumbani nikuwaadhibu mara dufu kwa makosa ambayo kimsingi si ya kwao moja kwa moja na mara zote!!!

TUENDELEE

Anonymous September 15, 2009 at 5:35 AM  

Adam,

Kwanza asante kwa kuleta mada hii muhimu kuhusu mustakhabali wa elimu katika nchi yetu. Kwa ujumla nakubaliana na mtazamo wa jumla wa Sera inayotarajiwa kutekelezwa, lakini mambo ya msingi ambayo sote tunapaswa kujiuliza juu ya uanzishwaji wa sera hizi kama yanazingatiwa. Kwanza je, kuna uchunguzi maalumu umefanywa kuhusu uwezo, mapungufu, matarajio yaliopo mbele yetu katika sekta ya elimu na hata kujua matatizo ambayo yanaweza kutokea kama mambo fulani muhimu hayatatekelezwa katika kusimamia sera za elimu Tanzania. Ni muhimu kujua uwezo wetu wa sasa katika kusimamia elimu na mapungu yaliopo, ili tunapoanzisha sera mpya iwe rahisi kuweka mkazo wa usimamizi katika maeneo ambayo tuna upungu nayo. Iwe ni uwezo wa kutambua vipaji, kutoa huduma ya chakula ama katika eneo lolote ambalo sera hii inatarajia kuleta mabadiliko. Eneo hili la uwezo wetu wa kusimamia elimu linagusa mambo mengi, je muundo wa utawala katika kutekeleza usimamizi mzuri wa elimu ukoje, je una nafasi ya kuruhusu utokaji na uingiaji wa taarifa kirahisi? tuhoji kuhusu ombwe iliyopo katika suala la uratibu, upangaji, mafunzo, na TEKNOHAMA je mambo haya yanaupungufu gani katika kuhakikisha elimu yetu ni salama katika ubora wake?

Pili ningependa kuona kama, sera hii inakuja baada ya kutambua ombwe kubwa la kuweza kuhudumia watanzania hawa ambao ndiyo watakao patiwa elimu hii, je nafadsi yetu ikoje katika sekta ya elimu, inaendana na mabadilko ya watu, mahitaji ya watu nan idadi ya watu wanaoongeza kuhitaji kupatiwa elimu hii. Ombwe iliyopo imetambuliwa, ili pamoja na kuleta sera hizi mpya hazitafanya kazi kama hatutakuwa tumetambua matatizo yaliopo katika mfumo wa sasa. Ni lazima, lakini sana ni muhimu kuyatambua haya ili hizi sera tunazoanzisha ziweze kufanya kazi na kuleta matunda tuanayo tarajia.

Mwisho kwa leo , je tunajua ombwe inayoletwa na uwezo wetu wa kifedha. Huu ni ombwe mbaya sana ambao unaweza kuathiri utekelezaji wa sera zetu. Sera hizi zitatekelezwa kwa fedha kutoka wapi? je ni mapato yetu ya Ndanin na kama ni fedha zetu tumejiandaa kwa kiasi gani kugharamia mabadiliko haya ya kisera? Na kama tunategemea fedha za nje, ni nani huyo ambaye anatoa fedha kwa ajili ya elimu ya watoto wetu, anaaminika vipi kwamba atatoa fedha hizo kwa wakati? Na je hatabadilika tukiwa kati kati ya utekelezaji na kutuancha soremba? Haya ni mambo muhimu matatu ambayo ndani yake yana maeneo muhimu ya kuangaliwa wakati wa kufanya uchambuzi wa hali yetu kwa sasa na kujua bayana kabisa wapi tuna nguvu ya kutosha, na wapi tuna mapungu na hivyo kuwa na nafasi kubwa ya kuweka juhudi yatu kuondoa mapungu na kuendelea kuboresha maeneo tunayo fanya vizuri.

Ni katika uchambuzi huu ndipo tunaweza kuweka vigezo vya namna ya kupima namna tunavyoendelea kutekeleza sera zetu kupitia mikakati na malengo mbalimbali tunayojipangia.

Tanzania, kupitia taasisi zake tuna kasumba ya kutofanya uchambuzi wa namna mifumo yetu inavyofanya kazi mpaka pale tu wageni wanapotulazimisha, hivyo tumeadhiri kwa kiasi kikubwa matokeo mazuri katika mipango yetu. je ni mfumo gani wa ufuatiliaji utawekwa bila kujua matatizo na ubora wetu uko wapi?

Mimi Andulile, mtoto wa mkulima , nawasilisha mawazo ambayo hayakupata nafasi ya kusikika.

Adam September 15, 2009 at 11:46 AM  

Oh ndugu yangu Andulile, nakushukuru sana kwa mchango huu mzuri. Umebainisha kwa kina masuala mbali mbali. Nitachangia kwa urefu wakati mwingine, kesho nikiweza.

Tuendelee kuchagia.
Karibu

SUBSCRIBE- Andika email yako hapa utumiwe habari mpya

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008 modified by Subi nukta77

Go Back to TOP