KUPANDA KWA BEI ZA NAULI NA ATHARI ZAKE KWA WANANCHI WENYE KIPATO CHA CHINI
Kupandishwa kwa gharama za
usafiri kumekuwa na mapokeo hasi kwa baadhi ya wadau jijini Mwanza, hasa
ukizingatia gharama za maisha kuwa juu, zaidi kwa watu wenye kipato cha chini.
Wakiongea na mwandishi wa makala
haya kwa nyakati tofauti tofauti, juu ya ni kwa jinsi gani wamepokea kauli
iliyotolewa na mamlaka ya uthibiti wa usafiri wa majini na nchi kavu (SUMATRA)
juu ya kupandishwa kwa nauli, wadau
tofauti tofauti walikuwa na maoni mbalimbali juu ya suala hilo
Bwana Gudluck John, mtumishi
katika sekta ya umma, anasema,
“nilipokea taarifa hiyo kwa mstuko sana ukilinganisha na hali ya maisha kuwa
ngumu. Kiwango kilichopandishwa ni kikubwa sana ukizingatia ukweli kuwa hali
hiyo itapandisha gharama za maisha
wakati misharaha haipandishwi.”
“Kwa sasa nitatakiwa kutumia TSH
800/= kwa siku kwa ajili ya usafiri, gharama ambayo kwa mweizi itakuwa
takribani TSH 24,000/=. Nikiongeza na nauli ya watoto wangu watatu, ambayo
itakuwa takribani TSH 37,000/=, kwa
mwezi nitakuwa natumia zaidi yaTSe3H
61,000/=; gharama ambazo ni kubwa sana ikiwa mshahara utabaki kuwa ule ule
ambao nilikuwa natumia nauli ya takribani 32,550/= kwa mwezi,” Bwana Gudluck
anafafanua.
Bibi Angela Willy, mkazi wa
Butimba na mtumishi katika sekta binafsi, anasema kuwa hofu yake kubwa ipo
kwenye upandaji wa bei za vyakula kutokana na gharama za usafirishaji. “Bajeti
yangu kwa ajili ya chakula itaongezeka kulingana na bei ya vyakula
itakavyopanda. Jambo ambalo litafanya maisha kuwa magumu kwani mshahara huo huo
niupatao ndio utatakiwa kugharamia gharama
hizo”, anasema Bi Angela.
“Serikali pamoja na waajiri
katika mashirika yasiyo ya kiserikali
watufikirie wafanyakazi, kutokana na gharama za maisha kupanda, kwa
kutuongezea mishahara ili tuweze kumudu hali hii” anashauri Bi Angel.
Hata hivyo, kwa kuhusu suala la
upandaji wa bei za vyakula, imeelezwa kuwa kupanda huko kwa nauli hakutoathiri
bei za vyakula katika masoko ya bidhaa hizo jijini kutokana na msimu wenyewe
kuwa ni wa mavuno.
Athuman Kalinga ni msafirishaji wa bidhaa mbalimbali za vyakula kutoka Bukoba
na kuzileta katika soko kuu jijini humo anasema kuwa, pamoja na kupanda kwa bei
za nauli yeye na wafanyabiashara wengine hawatoathirika kiasi cha wao
kupandishiwa gharama za usafirishaji wa bidhaa hizo kutokana na sababu kuwa
usafiri mkubwa wanaotumia ni kwa njia ya meli na kuwa gharama za usafirishaji
zinaendana na kiasi cha bidhaa zinazosafirishwa.
“Asilimia kubwa ya mchele unaouzwa
katika maeneo mbalimbali ya jiji hili ni kutoka Mwanza na shinyanga ambapo
husafirishwa kwa njia ya marori lakini maharagwe na mahindi hutolewa mkoani
Kagera ambapo husafirishwa kwa njia ya meli,” anafananua msafirishaji huyo.
Zaidi, Bwana Kalinga, ambae pia
ni mfanyabiasha wa bidhaa za chakula katika soko hilo, anaongezea kuwa ,kwa
aonavyo yeye, hali hiyo pia haitoathiri bei za vyakula. “Bidhaa za vyakula
haziwezi panda bei kwa sababu kipindi
hichi ni cha mavuno,” anasema.
Bwana kalinga ameendelea kusema
kuwa kwa sasa bei za mchele, kwa mfano, zimeshuka toka kiasi cha TSH 2000 kwa
KG moja na kuuzwa kati ya TSH 1700 na 1800; sababu kuwa msimu huu ni wa mavuno
kutakuwa na mchele mwingi sokoni, bei ya mchele haitoweza kupanda.
“ Kama unavyojua kama bei
imeshuka huko tunapochukua kwa mkulima hiyo haiwezi kutufanya kupandisha bei za
vyakula, ukiangalia maharagwe na mahindi tunanunua Bukoba na tunasafirisha kwa
meli lakini katika kusafirisha mzigo mkubwa kama tunaosafirisha melini wala nauli
yake haipandi kwa hiyo hatuwezi kupandisha bei” anasisitiza .
Dr. Odass Bilame, mchumi kutoka
chuo kikuu cha Mt. Augustine Tanzania (SAUT), amesema kuwa licha ya kuwa kwa
sasa ni msimu wa mavuno, baada ya msimu huu kupita kwa kiasi fulani gharama za
bei za vyakula zitapanda kutokana na upandaji huu wa nauli kuathiri gharama za
usafirishaji.
Pia, Dr. Bilame anaongezea kuwa
mfumuko wa bei utaathiri sana wananchi ambao kipato chao ni cha chini; tabaka
kati ya masikini na matajiri litaongezeka. “Mishahara, kwa mafano, wanayopewa
walimu ni midogo ukilinganisha na ya mawaziri. Hivyo, kupanda kwa bei za nauli
kutaathiri sana gharama za maisha yao na hivyo, kushindwa kutimiza malengo yao
ya kuwa na maisha bora,”anasema Dr. Bilame.
Hata hivyo, Dr. Bilame anatoa
angalizo kwa serikali kuwa inatakiwa kuangalia mfumuko wa bei wakati ikifanya
maamuzi ya bei za vitu kupanda, kama iilivyopandisha bei za nauli kwani mfumuko
wa bei unaathiri fursa endelevu za kiuchumi kwa wananchi na hivyo, kuikosesha nchi
yetu kushinda tuzo ya utawala na maendeleo ya uchumi katika nchi za Afrika.
Pia, anaishauri serikali kuwa na
mpango maalumu wa kuwashirikisha wadau mbalimbali kabla ya kufanya maamuzi ya
kupandisha nauli badala ya kufanya maamuzi hayo pekee yao.
Mwisho, Dr. Bilame aliitaka
serikali kupunguza kiwango cha kodi kwenye mafuta kwani ndio sababu kubwa ya
nauli kupanda.
kwa upande wa wasafirishaji, Dr.
Bilame anawataka waangalie uwezekano wa kununua vyombo vya usafiri vilivyovipya
ili kuondokana na gharama za kununua vipuri mara kwa mara kwa ajili ya vyombo
hivyo ambavyo ni chakavu.
Kupanda kwa bei za nauli
kulitangazwa mwanzoni mwa mwezi huu na SUMATRA, chombo chenye mamlaka ya
kisheria kufanya mapitio ya bei za nauli; bei hizo zimekwishaanza kazi rasmi
tangu jana tarehe 12/04/2013, licha ya wasiwasi unaoonekana katika jamii juu ya
kupanda kwa gharama za maisha na hivyo, kufanya maisha kuwa magumu zaidi kwa
baadhi ya watu, hasa wenye kipato cha chini.
0 comments:
Post a Comment