Kikwete Muunge Mkono Mwakyembe vita ya Mihadarati!
Kikwete Muunge Mkono Mwakyembe vita ya Mihadarati!
Mhakikishie ulinzi
Rais Kikwete. Chanzo- IPPMedia |
Moja ya jambo lililomletea sifa Rais
wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete ni kuzinduka usingizini na kupanga safu yake
ya watendaji iliyobora zaidi.
Miongoni mwa mawaziri wanaotajwa
kuwa madhubuti na makini katika utendaji wao ni Sospeter Muhongo, William Mgimwa
na Harrison Mwakyembe, na Naibu waziri January Makamba. Hawa wameungana na
mawaziri wengine waliokuwepo tangu mwanzo kama vile John Pombe Magufuli.
Uteuzi mzuri ni hatua muhimu japo
haijitoshelezi kukamilisha utendaji uliotukuka. Usimamizi na miongozo isiyo na
chengachenga ni muhimu zaidi kuhakikisha Mawaziri wanatekeleza wajibu wao
vizuri. Ndiyo maana katika Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa, mawaziri husika
wanakula kiapo (mkataba) wa kujifunga kuwajibika.
Dkt Harrison Mwakyembe, Waziri wa Uchukuzi, hivi karibuni
amejitokeza na kuweka msukumo mkubwa zaidi katika kukabiliana na aibu iliyolifika
taifa letu. Janga la miharadati.
Jambo hili linagusa wizara yake
moja kwa moja na hivyo anao uhalali wa kisheria kujitoa kwa dhati ya moyo wake
kukabiliana na jambo hili maana imethibitika kuwa uwanja wa ndege wa Kimataifa
wa Mwalimu Nyerere ni njia kuu ya kusafirishia madawa hayo huku kukiwa na madai
kuwa Bandari ya Dar es Salaam, ndiyo lango kuu la kuingizwa nchini madawa hayo.
Kujitokeza kwa Mwakyembe kumepeleka salamu nzito kwa Vigogo wa Unga
nchini na duniani. Rekodi ya Mwakyembe
iko wazi kwamba akilisimamia jambo huwa hafanyi makida makida wala kuigiza,
anamaanisha. Ndivyo wanaomfahamu wasemavyo. Janga hili la aibu kwa taifa
kuwa genge la wauza unga, kama ni kipele kimepata mkunaji. Ahsante Rais Kikwete
kwa kuipatia Tanzania mtu huyu kusimamia wizara hii.
Hata hivyo jambo hili ni la
hatari kubwa kama inavyojulikana duniani kuwa biashara hii inafanywa na mijitu
isiyokuwa na haya wala soni, mijitu isiyokuwa na utu bali iliyojaa damu
mikononi mwao. Ubabe wa wauza unga unaelezwa kuwa chanzo cha mamlaka mbali
mbali kunyamazishwa, ikiwemo mamlaka iliyokuu kabisa ya utumishi wa nchi.
Kujitokeza kwa Dkt. Mwakyembe ni
kujitoa mhanga maisha yake. Ni mfano wa uzalendo unaohitajika sana miongoni mwa
viongozi wetu. Hatua hii ya Mwakyembe inayaweka majukumu mazito mikononi mwa
Rais Kikwete. Na kusema ukweli ni hatua inayompa mtihani mkubwa Rais wetu,
maana ni lazima afanye kitendo kumuunga mkono mteule wake.
Moja ya jambo analoweza kufanya
Rais Kikwete ni kutangaza hadharani
kabisa tena mapema sana kuwa anaunga mkono jitihada za Wizara ya Uchukuzi chini
ya jemedari Dkt Mwakyembe. Hii itaongeza uzito wa salamu aliyotuma
Mwakyembe kwa vigogo wa unga.
Sambamba na kutangaza hadharani
kabisa kuunga jitihada za wizara ya uchukuzi, Rais pia hana budi kumhakikishia waziri wake ulinzi.
Usalama wa Mwakyembe ni suala nyeti la usalama wa taifa. Ni ishara ya mwanzo wa
ushindi wa taifa tukufu la Tanzania dhidi ya miharadati. Kwa hesabu za kawaida,
mashetani ya biashara ya unga, yatatamani sana kumuangamiza Mwakyembe ili
kuzidi kueneza hofu miongoni wa binadamu wa kipindi hiki.
Pia unyeti wa kumlinda waziri
Mwakyembe unatokana na historia ya maisha yake ambapo muda si mrefu alinusurika
kifo baada ya kudaiwa kulishwa sumu. Jambo hili ni nyeti zaidi sasa, maana
kudhulika kwake kokote hivi sasa kunaweza kuwa mwanzo wa kusambaratika kwa
taifa. Watanzania wanyonge na wapole
hawa wanaoumizwa na dawa za kulevya na madhila mengine wanaweza kuamua kuililia
damu ya kiongozi wao na tangu hapo hamkani haitokuwa shwari tena!
Nimefanya utafiti mdogo juzi na
jana kwenye mitandao ya kijamii, unaona wazi kabisa kuwa wasafirisha unga (punda),
vigogo wa unga pamoja na makuwadi na
walamba viatu wao, wamekazana kumkejeli na kumkatisha tama Mwakyembe. Unakutana
maneno kama vile “hana ubavu huyo, ni
mpenda sifa tu, hana lolote, anatafuta urais huyo”.
Kutoka thehabari.com |
Kama ni kutafuta sifa, basi Mwakyembe amechagua fungu lililojema, maana
analikabili suala ambalo likiachwa liendelee litaizamisha nchi! Kama ni
upenda sifa, basi natamani kila waziri akiwa mpenda sifa kwa namna hii na taifa
litaanza kung’aa tena badala ya kuzidi kufifia na kufubaa.
Aidha Rais Kikwete anayosababu
zaidi ya kutangaza kumuunga mkono waziri Mwakyembe. Habari zinahusisha kusuasua
kwake katika vita dhidi ya miharadati na kuhusika kwa familia yake katika
biashara hii. Taarifa zinabainisha kuwa mwanawe Rais Kikwete, ni miongoni mwa
vigogo wa unga nchini.
Taarifa za Ridhiwani Kikwete
kuhusishwa na dawa za kulevya si ngeni nchini. Zimeenea si haba. Na hata hivi karibu
ametajwa kwenye kinachoitwa kuwa barua kutoka kwa wafungwa wa kitanzania huko
Hong Kong! Haya yanaweza kuwa ni maneno tu ya waswahili sisi. Na maneno hata
kwenye khanga yapo.Lakini kule kumhusisha Ridhiwani, mtoto wa mtumishi mkuu wa
umma, si jambo la kufumbia macho.
Rais wetu anapaswa aoneshe kwa
vitendo kuwa hahusiki yeye wala familia yake. Moja ya njia za kuthibitisha hilo
ni kutangaza kumuunga mkono Dkt. Mwakyembe pamoja na wote wanaojitoa mhanga
katika kukabiliana na janga hili. Zaidi mhe. Rais awahimize mawaziri wengine wanaohusika kwa namna yoyote kama vile mambo ya ndani, maliasili na utalii waungane katika harakati hizi maana kidole kimoja kinavunja chawa kwa shida sana!Shime Rais wetu. Bado tumesaliwa na kaimani
kidogo nawe.
Ridhiwani Kikwete ktkt ya Rais wa China na Mkewe. kutoka blog ya Darmetropolitan |
2 comments:
'MWAKYEMBE ALINDWE' http://talkbongo.blogspot.com/2013/08/mwakyembe-alindwe.html
http://www.mwananchi.co.tz/habari/Kitaifa/Mwakyembe+apewe+ulinzi+wa+uhakika/-/1597296/1961690/-/jd83ok/-/index.html
Post a Comment