Kufungiwa Mwananchi, Mtanzania ni bonge la fursa
Kufungiwa kwa magazeti ya Mwananchi Mtanzania ni fursa chungu.
Serikali imeyafungia magazeti ya
Mwananchi na Mtanzania. Maumivu tena.
Lakini hayanabudi kutupata, ili tupone.
Sheria ya magazeti ya mwaka 1976
ilishatajwa na tume ya Francis Nyalali kwamba ni kandamizi na haistahili kuendelea
kuwepo katika hali hiyo iwapo Tanzania tunayoijenga ni ya kidemokrasia. Hii ilikuwa
ni mwanzoni mwa miaka ya 1990. Mpaka leo ni miaka mingapi? Nini cha maana
tulichofanya?
Natambua zimekuwepo jitihada za
hapa na pale za wanaharakati kushinikiza sheria hii kufutwa, lakini je
tumefanya ya kutosha?
Fursa ninayoiona hapa ni kwamba
tumepata nafasi kwa wakati mwingine wa kukasirika
na kujazbika na hivyo kupambana na hili dubwana! Kukaa na joka lenye sumu
hata kama halijakugonga bado na kukutia sumu yake ya kufisha, hakuondoi hatari
ya joka hilo. Litakuua wakati wowote.
Ni wakati mwingine kwa watanzania
wanaoipenda nchi yao kuungana na kushinikiza kufutiliwa mbali kwa vipengele
kandamizi kwenye sheria ya magazeti. Kimsingi sheria hiyo ni batili (japo sio
mwanasheria mimi) maana inapingana na katiba! Iweje mamlaka ya kutoa haki
yawekwe kwenye mikono ya chombo kisicho mahakama?
Tuitumie fursa hii kupigania haki
hii ya msingi katika kuimarisha demokrasia nchini.
Naiona fursa hapa ya kuanza kwa
vuguvugu na pambazuko jipya la kupambana na si sheria ya magazeti bali na
nyingine zote zaidi ya 40 zinazojulikana kuwa kandamizi. Msemo wa jeshi la
China unahusika sana hapa yaani kwamba Toka jasho jingi sana wakati wa amani,
ili umwage damu kidogo wakati wa vita.
Hakuna ziada mbovu.
Shime wana wa Tanzania. Tumetiwa kidole machoni. Natupambane sasa.