Pekua/search

Monday, September 30, 2013

Kufungiwa Mwananchi, Mtanzania ni bonge la fursa




Kufungiwa kwa magazeti ya Mwananchi Mtanzania ni fursa chungu.

Serikali imeyafungia magazeti ya Mwananchi na Mtanzania.  Maumivu tena. Lakini hayanabudi kutupata, ili tupone.

Sheria ya magazeti ya mwaka 1976 ilishatajwa na tume ya Francis Nyalali kwamba ni kandamizi na haistahili kuendelea kuwepo katika hali hiyo iwapo Tanzania tunayoijenga ni ya kidemokrasia. Hii ilikuwa ni mwanzoni mwa miaka ya 1990. Mpaka leo ni miaka mingapi? Nini cha maana tulichofanya?

Natambua zimekuwepo jitihada za hapa na pale za wanaharakati kushinikiza sheria hii kufutwa, lakini je tumefanya ya kutosha?

Fursa ninayoiona hapa ni kwamba tumepata nafasi kwa wakati mwingine wa kukasirika na kujazbika na hivyo kupambana na hili dubwana! Kukaa na joka lenye sumu hata kama halijakugonga bado na kukutia sumu yake ya kufisha, hakuondoi hatari ya joka hilo. Litakuua wakati wowote.

Ni wakati mwingine kwa watanzania wanaoipenda nchi yao kuungana na kushinikiza kufutiliwa mbali kwa vipengele kandamizi kwenye sheria ya magazeti. Kimsingi sheria hiyo ni batili (japo sio mwanasheria mimi) maana inapingana na katiba! Iweje mamlaka ya kutoa haki yawekwe kwenye mikono ya chombo kisicho mahakama?

Tuitumie fursa hii kupigania haki hii ya msingi katika kuimarisha demokrasia nchini.

Naiona fursa hapa ya kuanza kwa vuguvugu na pambazuko jipya la kupambana na si sheria ya magazeti bali na nyingine zote zaidi ya 40 zinazojulikana kuwa kandamizi. Msemo wa jeshi la China unahusika sana hapa yaani kwamba Toka jasho jingi sana wakati wa amani, ili umwage damu kidogo wakati wa vita.

Hakuna ziada mbovu.   
Shime wana wa Tanzania. Tumetiwa kidole machoni. Natupambane sasa.




0 comments:

SUBSCRIBE- Andika email yako hapa utumiwe habari mpya

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008 modified by Subi nukta77

Go Back to TOP