Pekua/search

Thursday, April 17, 2008

Mama Salma Kikwete aigwe. (Mjadala zaidi)


Mjadala huu hautafikia ukomo maana hata ufanyike utafiti wa namna gani unaohakikisha tena na tena na tena kwamba watu huwa bora zaidi wanapojifunza, kuwasiliana au kutumia lugha zao za kwanza, ukweli utabaki kwamba dola za magharibi zinazotumia lugha ya kiingereza bado zinatawala utamaduni wa kizazi kipya. Na si wote walioweza kujikomboa toka kwa kasumba ya ubora wa magharibi kwamba kuendelea, kuelimika na kustaarabika ni kuachana na asili zetu na kukumbatia umagharibi katika utamaduni hasa katika lugha.

Ni kweli kwamba katika dunia ya sasa ya utandawazi, kujua lugha za kimataifa kama kiingereza kuna manufaa zaidi. Ila lugha hizi zinatakiwa ziwe nyongeza siyo badala ya lugha za asili. Msisitizo lazima uwe kwa lugha ya kwanza na baada ya hapo mtu akijifunza lugha ya ziada, vyema.

Kwetu sisi uzalendo ni kuvutiwa na kuwaunga mkono watu wanaofanya juhudi kukuza kiswahili, bila kujali sababu zinazopelekea mapenzi yao na ustawi wa kiswahili.

Binafsi huwa nafurahishwa sana na viongozi wa nchi za kiarabu hasa raisi wa Misri wanavyopenda lugha zao na kuzitumia hata wanapokuwa katika mikutano na viongozi wa magharibi. Mojawapo ya mikutano hiyo katika Ikulu ya raisi wa Marekani, Hosni Mubarak akaanza tu hotuba yake kwa kiarabu huku inarushwa moja kwa moja na unaona nyuma maafisa wakihangaika kutafuta mtafsiri ila yeye hata hakusubiri apatikane akaendelea tu na hotuba yake. Hawa ni viongozi wachahce wenye ujasiri wa kutetea tamaduni zao kwa gharama ya kuonekana malimbukeni kwa watu wao wenyewe kama baadhi yetu wanavyomuona Salma.


To: wanazuoni@yahoogrou ps.com
From: ericbeda@gmail. com
Date: Thu, 17 Apr 2008 11:03:54 -0400
Subject: Re: [wanazuoni] JUU YA LUGHA

Wanazuoni,

Mjadala wa Lugha kama msukumo wa elimu na maendeleo imeshafanyika sehemu nyingi sana duniani na utafiti nyingi zilizofanywa zinaunga mkono wa kuwa kusoma au kutoa/kupokea elimu kwa lugha yako ya kwanza inasaidia kwa kiasi kikubwa kukuwa kwa uerevu wa mtu haswa kwa watoto chini ya miaka 14.

Sababu ya sisi watanzania kutokuthamini lugha yetu au kutokutumia lugha yetu katika mitaala yote na ngazi zote za elimu bado ni kitendawili kwangu mimi ila nadhani hizo sababu zinaweza kufanana na sababu za ingawa nchi za ulaya zinatoa ruzuku kwa wakulima wao sisi watanzania hatutowi(au haturuhusiwi kutoa) ruzuku kwa wakulima wetu, na ingawa kilimo kilikuwa (sina uhakika tena) kinachangia asilimia 80 ya uchumi wetu mitaala yetu elimu ya msingi ilibadirishwa (nadhani imeshawekwa sawa) na sayansi kilimo kikafutwa


On Thu, Apr 17, 2008 at 8:42 AM, bernard baha <bahabp2003@yahoo. com> wrote:

Amani kwenu wanazuoni,
Huu mjadala wa lugha mimi nilidhani umefikia ukomo na wote sasa tunaelewa jinsi ambavyo kutumia lugha za watu inavyokuwa taabu kuyafikia maendeleo. Sasa kumbe kamaradi Adam na Dada Catherine wamenifungua macho kabisa kwa kuuibua huu mjadala. Ebu nirejee kwanza katika baadhi ya hoja za dada yetu mpendwa Catherine,kwamba isingekuwa wasomi tusingepata uhuru,nadhani hoja yake hapa ni umahiri wa Mwl kwamba aliweza kuwakonga mioyo Waingereza na kuwashawishi kwamba tupo tayari kwa uhuru!
Nadhani hii hoja haijitosherezi kabisa ktk utetezi wake, ama ndiyo kusema kama tukiinyambua kimantiki kwamba bila kiingereza Tanganyika ingeendelea kuwa koloni! huu ni upotoshaji wa historia yetu na nafasi ya lugha ya kiswahili katika kuleta uhuru wa Tanganyika,hicho kiswahili cha wandengereko, wazaramo, na makabila uliyoorodhesha ama kusema watu wa ukanda wa Pwani sio tena mali ya kabila ama kundi fulani kama lugha za makabila mengine! tupo wengi tuliozaliwa katika Tanzania ya leo ambao lugha yetu ya kwanza ni kiswahili na tunaota na kufikiri kwa lugha hiyo! Lugha ya kiswahili ndio lingua franka ya Afrika ya Mashariki na Kati kama ilivyokuwa Kiinglishi kwa Ulaya na maeneo mengineyo.
kusambaa kwa lugha ni juhudi na jitihada za wenye lugha kuisambaza na kujivunia kuitumia na hivyo kuwafanya wengine wasioitumia wafikirie kuitumia pia,sasa vitendo vyetu ndio vinatuponza tunaukimbilia uingereza na kuona aibu kutumia kilicho chetu matokeo yake ndiyo haya mpaka leo tunapiga jaramba hatusongi mbele kama Taifa kimaendeleo
Kama ambavyo wao wanajifunza lugha zetu kwa ajili ya matumizi hata sisi twaweza fanya hivyo hivyo kwa lugha zao huku tukiweka mbele zaidi matumizi ya lugha yetu,pale inapolazimu ndio tutumie lugha zao.Lugha ni utamaduni wa taifa sasa kwa kufikiri kizungu vp ndio tutakuwa kama wao ama? Ndio maana Frantz Fanon alituasa kama tunafikiri hatujawa tayari kujitawala na kama tunaona kwamba Ulaya ama Uingereza ndio kwenyewe tusipoteze muda tuwalete Waingereza warudi kututengeneza ili tuufahamu vyema utamaduni wao na lugha yao wao wanjua vyema zaidi kuliko sisi! Shime jamani tuondokane na mawazo ya kudharau lugha yetu adhimu ya Kiswahili, Hata hivyo nakubali kutokukubaliana kwani kila mmoja ana mawazo na mitazamo yake kuhusu masuala ya kijamii,kiuchumi na kisiasa. Leo hii ukienda Ujerumani unaweza usipate huduma kama hutaongea kijerumani na hapo ni mlangoni na jirani sana na Uingereza.
Tuendeleze mijadala ya aina hii.
Wakatabahu.
Baha.

Chanzo: Wanazuoni yahoogroup

0 comments:

SUBSCRIBE- Andika email yako hapa utumiwe habari mpya

Enter your email address:

Delivered by FeedBurner

  © Blogger templates 'Neuronic' by Ourblogtemplates.com 2008 modified by Subi nukta77

Go Back to TOP