Mgomo wa madaktari ni darasa- Wako wapi Wanafunzi?
Udhaifu wa hoja si hoja, hoja ni tafakuri yake
Na Adam Gwankaja.
Makala haya yalichapishwa mwezi Februari kwenye safu ya Hoja dhaifu gazeti la AFRIKA LEO. Hata hivyo mgomo umekuwa nasi tena sasa kwa mara nyingine, hoja dhaifu katika makala haya bado zina mashiko, ni vema kuzirejea. Kama kawaida udhaifu wa hoja si hoja hoja ni tafakuri yake. Tuendelee kutafakari.
Mgomo wa
madaktari umetokea na madhila yake tumeyapata. Umekwisha rasmi kuelekea
mwishoni wa wiki iliyopita. Inaelekea hata madaktari wenyewe hawakuupenda, ila
ndiyo hivyo umetokea. Hatuwezi kurushia siku nyuma kuuzuia usitokee, tusipate
maumivu yaliyopatikana, lakini tunaweza kuutumia kuzuia uwekano wa kutokea
tena. Tunaweza kujifunza tukitaka.
Tunapofurahia
kwisha kwa mgomo wa wataalamu hawa huku tukigugumia maumivu tuliyoachiwa, ni
vema kutafakari hoja hii dhaifu ya mambo tunayojifunza kutokana na mgomo huu.
Naam mgomo huu
umekuwa darasa maridhawa kwa kila mwenye pumzi nchini. Ni darasa mwanana tena
ambalo ada yake ni kubwa, na tumeilipa japo stakabadhi hatukupewa wala
hatukudai.
Serikali yetu,
uongozi wetu na watawala wetu hapana shaka wamejifunza kuwa mabavu hayalipi.
Wamejifunza kuwa uziwi wa kuigiza hausadii maana hivi sasa ndiyo wenye kubeba
lawama nambari wani kwa yote machungu yaliyosababishwa na mgomo huu. Serikali
ikaweka kichwa ngumu kusikiliza kero za mabingwa hawa muhimu, mwishowe
ustahimilivu wao wa kawaida ukawashinda wakalazimika kuacha kufanya kazi
kuishinikiza serikali kusikiliza. Viongozi wakuu wa utumishi wa umma hapana
shaka wamejifunza kuwa ni muhimu kuwasimamia kwa karibu watumishi walioko chini
yao.
Warasimu watakuwa
wametambua kuwa jeuri halipi. Kusimamishwa kazi Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya
na Ustawi wa Jamii Blandina Nyoni na Mganga Mkuu wa serikali Deo Mtasiwa ni
salamu na ujumbe muhimu kwa warasimu wote kwamba cheo ni dhamana. Ni ushuhuda
muafaka kwamba hakuna mwenye mamlaka yasiyo ukomo.
Inakuwaje
katika mfumo mzuri wa uendeshaji taasisi za umma na utawala, Waziri Mkuu
asijulishwe matatizo makubwa yanaikumba taasisi nyeti kama Hospitali ya Taifa
ya Muhimbili hadi Madaktari Mabingwa wagome ndipo aambiwe? Warasimu
hawakuwajibika. Watakuwa wamejifunza na watatimiza wajibu wao pasipo kuendeleza
porojo kuwa wanaingiliwa na wanasiasa.
Madaktari na
watumishi wengine wa umma kama vile walimu hapana shaka mgomo huu umewapelekea
salamu kwamba licha ya maumivu kama kipigo na matusi, kebehi na kudharauliwa,
kusimamia haki zao, umoja na kujipanga hulipa.
Licha ya
madhila ya siku hizi takribani 17 za mgogoro, kusimama kwao kidete, madaktari
wameweza kulazimisha serikali si kuwasikiliza tu bali kuanza kuchukua hatua za
kutatua kero zao nyingi zikiwa za msingi katika utoaji wao huduma.
Kisingizio cha
kawaida cha serikali ni bajeti finyu. Sasa mbona baada ya kubanwa imeweza
kupandisha posho za madaktari kutoka shilingi 10,000 hadi kati ya shilingi
25,000 na 35,000 tena ndani ya bajeti ya mwaka huu wa fedha? Somo la vipaumbele
hapa linahusika sana. Serikali isipotaka kuweka vipaumbele kwa masuala ya
msingi, basi ilazimishwe kufanya hivyo kwa maslahi ya taifa kama ilivyotokea
katika mgogoro huu.
Na kwa
watanzania wote pamoja na wanaharakati somo liko wazi kuwa kuchekea udhalimu
hailipi. Tunajifunza kuwa tukisimama pamoja na kusema hapana kwa udhalimu na
manyanyaso basi vitakoma. Nguvu iliyoongezwa na maandamano ya wanaharakati kuishinikiza
serikali kusikiliza na kuyafanyia kazi madai ya madaktari haiwezi kupuuza
katika kutufikisha tulipofikia ambapo madaktari wamekubali kurejea kazini.
Na kwa upande
wa pili tamko la msisitizo la madaktari kutaka wanaharakati waliotiwa msambweni
kwa kutumia haki yao ya msingi nay a kikatiba kuandamana kueleza hisia zao
waachiwe pia haliwezi kupuuzwa tamko hilo katika kuachiwa kwa watanzania hao,
raia wema.
Migogoro ya
aina hii inayohusisha kudai haki za kundi fulani la jamii ni kama mtego wa
panya ambamo wanaingia waliokuwemo na wasiokuwemo. Sote tunapaswa kuwa na nia
moja. Tuendelee jufunza wingi wa elimu iliyomo kwenye matukio ya aina hii,
itusaidie kuboresha maisha yetu nchini. Udhaifu wa hoja si hoja hija fakuri
yake. Tuonane juma lijalo.
0 comments:
Post a Comment