Buriani Mwanaharakati Bi Shida Salum
Buriani Mwanaharakati Bi Shida Salum
Safari ya Shida Salum katika dunia hii iliyojaa
dhiki na simanzi imefikia tamati. Amepumzika sasa. Kadri historia ya Taifa hili
inavyoandikwa upya Watanzania tutamkumbuka kwa mengi.
Hakika Shida Binti Salum alizivaa na kuzimudu kofia
nyingi. Alikuwa mzazi, mwanasiasa na mwanaharakati. Wapo wanaomjua zaidi kama
mzazi. Pia wapo wanaomfahamu zaidi kama mwanasiasa. Tupo na tunaomtambua zaidi
kama mwanaharakati.
Nilikutana naye kwa mara ya kwanza mnamo mwaka 2006
wakati tuliposhirikiana katika utafiti wa
taasisi ya HakiElimu kuhusu haki ya kupata taarifa/habari. Alikuwa
akitokea kwenye mtandao wa asasi zisizo za Serikali za Kigoma na Kasulu
unaojulikana kama Kigoma and Kasulu Non-Governmental Organizations Network (KIKANGONET).
Wakati huo sikuwa namfahamu mtoto wake, Zitto Kabwe, ambaye nilikuja kumsikia
kwa mara ya kwanza mwaka 2007 baada ya wanaharakati wa Mtandao wa Jinsia
Tanzania (TGNP) kuandaa
maandamano ya kumuunga mkono katika viwanja vya Mabibo kufuatia kutolewa kwake
nje ya ukumbi wa Bunge baada ya kuibua tuhuma nzito kuhusu ufisadi wa Mgodi
wetu wa madini wa Buzwagi. Kwa lugha tunduizi ya Kifeministi, hii ina maana
nilimfahamu Shida kama yeye - Shida Salum - kabla ya kumfahamu kama Mama Zitto
kwa kuhusianishwa na umaarufu mkubwa aliojizolea mwanae katika medani ya
kisiasa nchini.
Tunapomkumbuka Shida kama mzazi aliyemlea
mwanasiasa mashuhuri pia tusisahau kumkumbuka kama mwanaharakati mahiri
aliyeendesha harakati na wenzake kama yeye na kupata ukubali katika jumuiya za
wanaharakati kama yeye na si (tu) kama mzazi wa fulani. Katika harakati za
kutafuta haki ya kupata taarifa, alishiriki kudhihirisha kiutafiti ni jinsi
gani watu wa kawaida, wakiwamo wenye ulemavu, wanakosa fursa ya kupata taarifa
muhimu kwa ajili ya umma. Cha kusikitisha ni kuwa hata taasisi zisizo za
kiserikali ambazo zinajiona ziko kiharakati zaidi na bora kuliko taasisi za
kiserikali nazo hazikuwa mstari wa mbele katika kutoa taarifa muhimu kwa
wananchi pale wanapofika kwenye ofisi zao au hata kutuma maombi kwa barua ama kwa
kupiga simu.
Katika harakati huyu ndiye Shida
tuliyemfahamu. Mwombolezaji mmoja katika mtandao wa Wanazuoni
aliyewahi kufanya kazi katika taasisi ya HakiKazi
anamkumbuka hivi:
"Nilimfahamu Bi Shida Salum kama Mwanaharakati tokea
Kigoma na kisha hapa Dar na Dodoma kwenye harakati zake za kutetea Watanzania
wenye ulemavu na maendeleo kwa ujumla. Ameacha legacy."
Hii
"legacy" yake, ama kumbukumbu ya kupigiwa mfano kwa tafsiri ya haraka
haraka, tuienzi katika harakati za kuyafanya maisha ya kila Mtanzania
- mdogo ama mkubwa, mwenye ulemavu au asiye na ulemavu, mwanamke na
mwanaume - yawe bora (zaidi na zaidi).
Nilipomkuta amekaa mbele ya banda alilokuwa
akilisimamia katika maonyesho pale katika Viwanja vya Mnazi Mmoja sikujua kuwa
hiyo ndio itakuwa mara yangu ya mwisho kuongea naye. Shida niliyemkuta
hospitalini AMI, japo hatukuongea, sauti yake bado ilikuwa ya mwanaharakati
asiyekata tamaa, akipambana vikali na moja ya vile ambavyo mmoja wa waasisi wa
Taifa letu changa la Tanzania aliviita maadui (wakuu) watatu wa maendeleo
(yetu).
Ingawa hatutamsikia akipaza sauti yake mwenyewe
katika Bunge Maalum la Katiba na maeneo mengine akiwakilisha kundi la wenye
ulemavu, sauti hiyo itasikika kupitia wale aliowaachia makabrasha au
waliompokea kijiti. Lakini tusiwaachie tu kina Fredrick Msigallah jukumu nyeti
la kutetea na kudai haki hizi ambazo, kwa namna moja au nyingine, zinatuhusu
hata na sisi ambao hatuna, ama tunaojiona hatuna, ulemavu. Na moja ya haki (za
kiraia) za watu walio na ulemavu ni kushiriki kikamilifu katika siasa kwa maana
ya kuongoza, kuwakilisha, kupigiwa na kupiga kura n.k.
Maisha ya Shida ni kielelezo tosha kuwa mwanamke
mwenye ulemavu anaweza kuwa mzazi, mwanasiasa na mwanaharakati. Tunapojiandaa
na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 tukumbuke pia kurekebisha masuala tete na tata
yaliyoibuliwa na utafiti huu wa CCBRT kuhusu changamoto za ushiriki wa watu wenye
ulemavu katika uchaguzi wa 2010 ambao kwa kweli ulinifungua sana macho. Kwa
kufanya hivyo tutakuwa tunaenzi harakati zake.
Kigoma mpokee mwanao. Binti wa Tanzania. Mtoto wa
Afrika.
Buriani Shida Binti Salum.
Imeandikwa na Mwanazuoni Chambi Chachage http://udadisi.blogspot.co.uk/2014/06/buriani-shida-binti-salum.html
Naam Nenda Mwanaharakati Shida Salum. Umemaliza safari https://www.youtube.com/watch?v=mrxFySY45wc
0 comments:
Post a Comment